Rais Kikwete haudhuria mkutano wa biashara Malaysia
Mkutano huo ambao umekuwa unafanyika kila mwaka kwa miaka 16 sasa tokea mwaka 1995, unatokana na uamuzi wa wakuu wa nchi za Jumuia ya Madola uliofanyika Cyprus mwaka 1993 na kuzinduliwa rasmi katika mkutano wa wakuu, uliofanyika Auckland, New Zealand mwaka 1995.
Mkutano huo huzungumzia masuala mbali mbali ya maendeleo na hasa umuhimu wa uhusiano mzuri kati ya Serikali, sekta ya umma na sekta binafsi katika kuleta maendeleo. Mkutano wa mwaka huu umepangwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Putrajaya (PICC) kilichoko katika mji mpya wa shughuli za Serikali ya Malaysia ulioko Patrajaya, nje kidogo ya mji wa asili wa Kuala Lumpur.
Nchi ya Malaysia imewaalika wakuu 25 wa nchi mbali mbali duniani kushiriki katika mkutano huo japokuwa haitarajiwi wote kushiriki mkutano huo. Kutoka Afrika amealikwa Rais Kikwete, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Omar El Bashir wa Sudan na Waziri Mkuu wa Lesotho.
Rais Kikwete atanawasili Malaysia kuhudhuria mkutano huo akitokea Shelisheli ambako alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Taifa la Shelisheli.
Mbali na kuhudhuria mkutano huo atazungumza kwenye kikao cha ufunguzi na pia kwenye kikao kitakachozungumzia namna mbadala na za ubunifu zaidi za kupata fedha kwa ajili ya maendeleo, Rais Kikwete pia atakuwa na shughuli nyingine muhimu za kikazi.
Miongoni mwa shughuli hizo ni Rais Kikwete kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Malaysia, Dato’ Sri Mohammed Tun Abdul Razak, kukutana kwa mazungumzo na aliyekuwa waziri mkuu wa Malaysia, Mheshimiwa Tun Dkt. Mahathir Mohamad, Rais wa Heshima wa Taasisi ya Uongozi ya Perdana Leadership Foundation.
Rais Kikwete pia atakutana na kula chakula cha usiku na wenyeviti, marais na watendaji wakuu wa makampuni makubwa ya Malaysia wakiongozwa na Mheshimiwa Mahathir Mohamed.