WAZIRIMkuu wa Denmark, Mheshimiwa Helle Thorning-Schmidt aliwasili nchini Machi 5, 2013, kuanza ziara ya siku nne ya Kiserikali katika Tanzania kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete. Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mjini Dar Es Salaam, Mama Helle Thorning-Schmidt amelakiwa na mwenyeji wake Rais Kikwete na viongozi wengine wa Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa Denmark.
Shughuli ya kwanza ya Waziri Mkuu huyo wa Denmark leo asubuhi itakuwa kukutana kwa mazungumzo ya faragha na rasmi na Rais Kikwete Ikulu, Dar Es Salaam, mazungumzo ambayo yatafuatiwa na viongozi hao wawili kuzungumza na waandishi wa habari. Baadaye mchana, Bi. Helle Thorning-Schmidt atatoa mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na jioni atahudhuria na dhifa ya kitaifa ambayo itaandaliwa na Rais Kikwete.
Keshokutwa, Bi. Thorning-Schmidt atakwenda Arusha ambako atatembelea Mahakama Maalum ya Uhalifu ya Rwanda (ICTR), atatembelea Kijiji cha Wamasai cha Lepurko na baadaye kutembelea shamba la kahawa linalomilikiwa na Bwana Christian Jespen.
Ijumaa, mama huyu atatembelea Hospitali ya Wilaya ya Mbulu na kituo cha kufundishia wauguzi cha hospitali hiyo, atatembelea Mbuga ya Wanyama ya Tarangire, atatembelea Makao Makuu ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na kukutana kwa mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Mheshimiwa Richard Sezibera kabla ya kutembelea Kituo cha Mafunzo cha Action Aid kinachoendeshwa na Serikali ya Denmark cha MS-TCDC. Mheshimiwa Helle Thornig-Schimidt ataondoka usiku wa siku hiyo kurejea nyumbani.