Na Mwandishi Maalum
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhakikisha kuwa Balozi mbali mbali za Tanzania nje ya nchi zinakuwa na Waambata wa Elimu kwa nia ya kukabiliana na kutatua matatizo ya wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika nchi mbali mbali duniani.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa moja ya wajibu mkubwa wa mabalozi wanaoziwakilisha Tanzania nje ya nchi ni kutetea na kulinda maslahi ya Watanzania walioko katika nchi hizo, bila kujadili kama Watanzania hao wamepelekwa nje na Serikali ama wamekwenda huko kwa njia nyingine.
Rais Kikwete amefanunua mambo hayo wakati alipozungumza na viongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu Algeria, nchi ambayo Rais Kikwete anaitembelea rasmi kwa siku tatu kuanzia Mei 9, 2015. Tanzania ina kiasi cha wanafunzi 370 wanaosoma Algeria. Rais Kikwete alizungumza na viongozi hao wanafunzi kwenye siku ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Kiserikali katika Algeria, Mei 9, 2015.
Akizungumza na viongozi hao wa wanafunzi, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania ina wanafunzi wengi katika nchi mbali mbali duniani, wanafunzi ambao wanahitaji huduma mbali mbali za kibalozi na hivyo ni lazima itafutwe namna ya kurejea katika utaratibu wetu wa zamani wa kuwa na Waambata wa Elimu katika balozi mbali mbali za Tanzania nchi za nje.
“Ni lazima tuwe na Waambata wa Elimu kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya vijana .wanafunzi wetu nje ya nchi. Kila ninapokwenda nakabiliana na matatizo kama haya mnayoniuliza nyie na mengine mengi na ya aina mbali mbali ya wanafunzi,” Rais Kikwete amwaambia wanafunzi hao mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Kuhusu nafasi ya mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi za nje, Rais Kikwete amesema kuwa ni shughuli muhimu ya kila balozi wa Tanzania katika nchi mbali mbali kushughulikia matatizo ya Watanzania.
“Mabalozi wetu kushughulikia matatizo ya Watanzania ni wajibu wao iwe ni wale Watanzania wanaopelekwa nje na Serikali ama wale ambao kwa njia moja ama nyingine wamejikuta nje ya nchi hata kama hawakupelekwa na Serikali. Huu ndio wajibu wa kila balozi wa Tanzania popote alipo,” amesema Rais Kikwete.
Wakati huo huo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa ilikuwa ni lazima kuanzisha Shule za Sekondari za Kata nchini kwa sababu mwaka 2005 ni asilimia sita tu ya wanafunzi waliokuwa wanainga sekondari kutoka shule za msingi nchini.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa katika miaka 10 iliyopita, yamekuwepo maendelea na mafanikio makubwa katika hali na hadhi ya shule hizo za sekondari za kata kiasi cha kwamba sasa shule hizo zimeanza kushindana na hata wakati mwingine kuzipiku shule binafsi na zile za serikali.
Rais Kikwete ametoa ufafanua huo usiku wa Mei 9, 2015, wakati alipozungumza na viongozi wa wanafunzi wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu katika Algeria kwenye siku ya kwanza ya ziara yake rasmi ya Serikali ya siku tatu katika nchi hiyo rafiki mkubwa na wa miaka mingi wa Tanzania.
Akijibu maswali ya wananchi hao , mojawapo likiwa kuhusu hali na hadhi ya sekondari za kata nchini, Rais Kikwete amesema kuwa ilikuwa ni lazima kuanzisha shule hizo kwa sababu nafasi za watoto wa shule kutoka shule za msingi hadi sekondari zilikuwa zinyu sana.
“Mwanzoni hali ilikuwa mbaya sana na hivyo uamuzi ulikuwa ni lazima kubadilisha hali hiyo. Ni asilimia sita tu ya watoto wetu walikuwa wanakwenda sekondari kutoka shule ya msingi katika nchi yenye watu wanaokaribia milioni 50 kwa sasa. Hali hii haikukubalika. Wajibu wetu, kama serikali, ilikuwa kutoa fursa kwa watoto wetu kupata nafasi nyingi zaidi za kuingia sekondari na tumefanikiwa sana katika hili,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Na wala siyo siri kuwa mwanzoni shule hizo zilikabiliwa na changamoto nyingi. Hatukuwa na walimu wa kutosha, vitabu vilikuwa havitoshi, Lakini sasa hali imebadilika. Walimu wa masomo ya sanaa sasa wanatosha na baadhi ya shule zina walimu wa ziada. Vitabu vimeanza kutosha.”
Aliongeaza Rais Kikwete: “Mwaka jana, kwa mfano, shule tatu bora za Mkoa wa Kilimanjaro, mkoa ambao umepiga hatua kubwa katika elimu, zilikuwa shule za kata na zote zilikuwa za Wilaya ya Mwanga.”
Rais Kikwete yuko katika Algeria kwa ziara rasmi ya Kiserikali ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Abdelaziz Bouteflika Mei 9, 2015.