Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Novemba 7, 2011, amekutana na kufanya mazungumzo na Mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles na Mkewe, Mama Camila, the Duchess of Cornwall.
Prince Charles na ujumbe wake amewasili Ikulu, Dar es Salaam, kiasi cha saa 4:10 kwa ajili ya mkutano na mazungumzo na Mheshimiwa Rais Kikwete ikiwa ni shughuli ya kwanza ya Mtoto huyo wa Malkia katika ziara yake ya siku tatu katika Tanzania.
Prince Charles na ujumbe wake aliwasili nchini jana, Jumapili, Novemba 6, 2011, akitokea Afrika Kusini, na yuko nchini kwa mwaliko wa Serikali ambayo awali ilikuwa imemwalika kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru mwezi ujao. Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza Desemba 9, mwaka 1961.
Akiingia Ikulu kutokea lango la Mashariki la Jengo hilo, Prince Charles ambaye amepokewa na Rais Kikwete kwenye lango hilo, amelakiwa kwa shamrashamra na vifijo na watumishi wa Ikulu pamoja na kundi kubwa la watoto wa shule za sekondari za Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na Prince Charles wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza na masuala mengine yanayohusu shughuli za kijamii.
Rais Kikwete amemshukuru Prince Charles kwa kukubali mwaliko wa kutembelea Tanzania akisisitiza hali nzuri sana ya uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza.
“Uingereza ni mshirika wetu mkuu katika mambo mengi. Uhusiano wetu ni mzuri sana. Uingereza ndio mshirika wetu mkuu katika shughuli za biashara. Uingereza ndio mwekezaji mkuu katika uchumi wetu na Uingereza ndio chimbuko kubwa zaidi la watalii wanaotembelea nchi yetu,” Rais Kikwete amemwambia Prince Charles ambaye amekaa Ikulu kwa kiasi cha dakika 50.