Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Machi 31, 2012, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Bi. Mary Consolata Muduuli.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Bi. Muduuli ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB kwa nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Seychelles, Rwanda, Ethiopia na Eritrea, alifuatana na Mwakilishi wa Benki hiyo katika Tanzania. Bi. Tonia Kandiero na mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, Bi. Salma M Salum.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete ameishukuru AfDB kwa misaada mingi ya maendeleo ambayo Benki hiyo imekuwa inatoka kwa Tanzania, na ameitaka kuendelea kusaidia jitihada za Watanzania kujiletea maendeleo.
Benki hiyo ambayo ilianza shughuli zake katika Tanzania mwaka 1971 hadi mwishoni mwa mwaka jana ilikuwa imeidhinisha miradi 121 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni tatu katika sekta za miundombinu, usafirishaji, kilimo, maji, huduma za kijamii, umememe, viwanda na madini na mawasiliano.
Tokea Machi mwaka huu, 2012, AfDB imeidhinisha miradi 16 ambayo 14 kati yao imeanza kutekelezwa na miwili bado haijaanza kutekelezwa. Miongoni mwa miradi miwili ambayo haijaanza kutelekezwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa njia ya kusambaza umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga.
Kati ya miradi hiyo 16, asilimia 34 ni ya sekta ya ujenzi wa barabara, asilimia 13 ni ya kilimo, asilimia 12.5 ni ya maji, asilimia 11.2 ni ya nishati ikifuatiwa na ile sekta za afya, elimu. Sekta nyingine zinachukua asilimia 18.7 kati ya miradi hiyo.
Miongoni mwa miradi mikubwa ya barabara ambayo inagharimiwa miongoni mwa miradi hiyo 16 ni ule wa ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma yenye kilomita 260 na ule wa ujenzi wa barabara ya Tunduru-Namtumbo yenye kilomita 193.
Wiki ijayo, miradi ya kufufua ujenzi wa barabara za Dodoma-Babati na Mangaka-Tunduru iliyocheleweshwa kwa sababu mbali mbali, itawasilishwa kwenye Bodi ya AfDB.