Rais Kikwete Azitaka Halmashauri Kutenga Ardhi kwa NHC

Baadhi ya nyumba za gharama nafuu zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

Baadhi ya nyumba za gharama nafuu zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)


RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameziagiza Halmashauri zote nchini kutenga ardhi kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya kujenga nyumba za bei nafuu kote Nchini. Rais Kikwete ametoa maagizo hayo leo mjini Tanga wakati akifanya majumuisho ya ziara yake katika Mkoa wa Tanga.

Rais amesema nyumba za bei nafuu zikijengwa zitatoa nafuu na kuondoa tatizo la makazi kwa wafanyakazi na wananchi wenye nia ya kumiliki nyumba na pia itapendezesha Halmashauri hizo. Katika ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga ambayo imefanyika kwa awamu mbili, Rais ametembelea Wilaya zote za Handeni, Kilindi, Lushoto, Korogwe, Mkinga, Muheza, Pangani na Tanga.

Rais pia amewataka viongozi kote nchini kusimamia na kuhakikisha kuwa tatizo la watoto kutomaliza shule linasimamiwa na kushughulikiwa ipasavyo kwa sababu huo ndiyo msingi wa maendeleo katika Taifa letu. “Viongozi lazima kusimamia suala la elimu kwani hapo ndipo tunapowekeza kwa ajili ya hatma ya vizazi vyote” amesema na kuongeza kuwa wasiokuwepo shule watafutwe na wazazi waulizwe walipo watoto hao walioacha shule. Rais amezitaka Halmashauri zote zikae na kujadili hali ya mahudhurio ya watoto shuleni na kutoa taarifa Serikali Kuu mapema.

Akiwa Mkoani Tanga, Rais amesema Serikali itaendelea kutekeleza ahadi zake na kusimamia zilizoanza ili zikamilike kwa wakati. Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu, Rais Kikwete amesema hatma yake iko katika matokeo ya maamuzi ya Bunge la Katiba na pia kutegemea aina gani ya serikali itakayopendekezwa, ambapo kama Bunge la Katiba litaamua kuwa na Serikali mbili, uchaguzi unaweza kusogezwa mbele kidogo kwa ajili ya matayarisho na kisha kufanyika, ila kama itaamuliwa kuwa na Serikali tatu, uchaguzi huo utategemea Katiba ya Tanganyika ambayo itabidi iandikwe kwanza. Rais Kikwete amerejea Dar-es- Salaam mara baada ya majumuisho.