Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Aprili 11, 2013 amezindua Mradi Kabambe wa Ukarabati na Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza Umeme uliogharimiwa na Shirika la Marekani la Misaada kwa Nchi Zinazoendelea wa Millenium Challenge Corporation (MCC) kwa mabilioni ya fedha na ambao utawanufaisha maelfu kwa maelfu ya wananchi.
Mradi huo ni moja ya miradi mingi inayotekelezwa kwa gharama ya msaada wa dola za Marekani milioni 698 (sawa na sh 1.9 trilioni) wa Shirika la Marekani la Millenium Challenge Corporation (MCC) katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na mmoja Zanzibar, katika wilaya 24, vijiji 356 na yeye kilomita 2,700, ikiwa ni kilomita 1,335 za Msongo wa Kati na kilomita 1,368 za Msongo Mdogo.
Sherehe za uzinduzi wa Mradi huo zimefanyika katika Kijiji cha Mkoka, Wilaya ya Kongwa, Mkoani Dodoma, zaidi ya kilomita 100 kutoka mjini Dodoma kwenye barabara iendayo Kiteto, mkoa wa jirani wa Manyara.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na mamia ya wanakijiji na wakazi wa vijiji vya jirani na Mkoka na miongoni mwa watu wengine waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais, Mohamed Gharib Bilal, Mtendaji Mkuu wa MCC Bwana Daniel Wolde Yonannes, Balozi wa Marekani katika Tanzania Mheshimiwa Alfonso Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa Millenium Challenge Account- MCA (Tanzania) Bwana Bernard Saidi Mchomvu.
Wengine ni Naibu Mawaziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene na Stephen Maselle, viongozi wengine wa Wizara na viongozi wa Mkoa wa Dodoma. Viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wajenzi wa mradi huo, M/S Pike Tanzania LLC, kampuni ambayo imetumia fedha yake binafsi kuiwekea umeme Shule ya Hogolo katika Wilaya ya Kongwa ikiwa ni mchango wa kampuni hiyo katika mradi huo, pia wamehudhuria sherehe hizo.
Mradi huo wa kusambaza umeme ni moja ya miradi inayojengwa na kutekelezwa na MCC katika Mikoa 10 ya Dodoma, Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Kigoma, Mwanza, Manyara, Njombe na Geita kwa gharama ya dola za Marekani milioni 698.
Mikoa hiyo ya Tanzania Bara ni mbali na mradi wa kutandaza nyaya chini ya Bahari ya Hindi kwa ajili ya kuvusha umeme kutoka Bara kwenda Zanzibar. Mradi huo wa Zanzibar ulizinduliwa jana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Mradi huo wa umeme ambao utanufaisha wananchi katika mikoa ya Dodoma na Manyara ikiwa ni wanufaika wa vijiji 20 katika Wilaya ya Dodoma Mjini, sita katika Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, vijiji vinne katika Wilaya ya Kondoa, vijiji vitano katika Wilaya ya Mpwapwa, 11 katika Wilaya ya Kongwa ikiwa ni pamoja na Kijiji cha Mkoka ambako sherehe za uzinduzi zimefanyika.
Vingi kati ya vijiji hivyo 46 vitakuwa vinapata umeme kwa mara ya kwanza katika historia vikiwamo vijiji 16 katika Wilaya ya Kongwa ambavyo vimepata umeme kwa mara ya kwanza katika miaka 50 ya historia ya Tanzania. Hadi mwezi uliopita, kiasi cha wateja wapya 1,300 wa kutumia umeme nyumba zao zilikwishaunganishwa na umeme katika Mkoa wa Dodoma.
Katika Mkoa wa Dodoma peke yake, mradi huo umeshirikisha ujenzi wa miradi midogo 38 na umegharimu dola za Marekani 17.8 sawa na Sh. Bilioni 28.5 ambako maelfu kwa maelfu ya wananchi watanufaika na kuboresha maisha yao kwa namna ambayo haijapata kushuhudiwa katika maisha yao.
Kuzinduliwa kwa mradi huo mkubwa wa kusambaza umeme katika vijiji vya Tanzania ni moja ya jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa asilimia ya Watanzania wanaopata huduma ya umeme inaongezeka kutoka asilimia 21 ya sasa hadi asilimia 30 mwaka 2015.
Aidha, kuzinduliwa kwa mradi huo kutainua kiwango cha ubora wa maisha ya wananchi katika vijiji hivyo kwa maana ya kuwapatia maji safi na salama, kuwapatia mwanga, kuwapatia uwezo wa kuendesha mashine, kuwezesha watoto wa shule kujisomea wenyewe usiku.
Miradi ya MCC ilianza kutekelezwa mwaka 2006 na makubaliano rasmi ya kutekelezwa kwa Mradi huo yalitiwa saini na Rais Kikwete na aliyekuwa Rais wa Marekani Mheshimiwa George W. Bush wakati alipotembelea Tanzania Februari 2008.
Miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya MCC iko katika maeneo matatu makuu ya Miundombinu. Eneo la kwanza ni la usafirishaji ambalo linajumuisha ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za Tanga-Horohoro, Tunduma-Sumbawanga, Namtumbo-Songea, Peramiho-Mbinga na kilomita 35 za barabara za vijiji vya Kisiwa cha Pemba na uwekaji lami katika Uwanja wa Ndege wa Kisiwa cha Mafia.
Eneo la pili ni la sekta ya maji lenye miradi miwili. Miradi hiyo ni ule wa ujenzi wa mtambo mpya wa kusukuma maji kutoka Ruvu Chini kwa ajili ya wakazi wa Jiji la Dar Es Salaam na mji wa Bagamoyo na ujenzi na ukarabati wa mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa maji safi na salama katika mji wa Morogoro.
Eneo la tatu ni sekta ya nishati ambayo Mradi wa Dodoma na Kiteto uliozinduliwa leo ni sehemu yake. Miradi mingine inayoendelea kutelezwa iko katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Kigoma na Mwanza na pia inagusa mikoa ya Njombe, Geita na Manyara.
Miradi hiyo ilichaguliwa na Serikali ya Tanzania yenyewe baada ya kuwa imefanikiwa kuvuka viungo muhimu vya kupata sifa za kupatiwa msaada huo wa Marekani.
Hata kabla ya Tanzania haijapewa kiasi cha dola 698 za kutekeleza miradi hiyo, tayari MCC iliipa Tanzania dola za Marekani milioni 11 kwa ajili ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi hiyo. Fedha zote hizo zimetolewa na Marekani kama msaada kama itakavyokuwa kwenye MCC ya pili ambayo maandalizi yake yameanza.
Ili kuweza kupata sifa za kupokea msaada huo wa Marekani chini ya MCC ambayo ilianzishwa na Utawala wa Rais Bush kugharimia maendeleo ya nchi zinazendelea duniani ikiwa ni jaribio la utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) Tanzania ililazimika kujipatia sifa kwa masharti 17.
Miongoni mwa masharti hayo ni nchi yoyote kuthibitisha kuwa inaendeshwa kwa utawala bora, inaendeshwa kwa demokrasia, inapambana kweli kweli na rushwa, na ina Serikali ambayo inawekeza kwa namna ya wazi kabisa katika maendeleo ya wananchi wake. Kwa sababu ya sifa zake kubwa, Tanzania ndiyo nchi ambayo ilipata msaada mkubwa zaidi kuliko nchi nyingine yoyote chini ya MCC.