RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Januari 9, 2013, amefungua miradi mingine miwili kwenye siku ya nne ya ziara yake ya siku tano ya shughuli nyingi za kikazi Mkoani Tabora.
Rais Kikwete ambaye aliwasili Mkoani Tabora Jumamosi iliyopita kwa ziara ya siku tano, amekuwa anafungua, kuzindua ama kuweka jiwe la msingi la miradi mbalimbali katika wilaya za Igunga, Nzega, Tabora Manispaa, Uyui na katika wilaya za Urambo na Kaliua.
Katika sherehe iliyofanyika eneo la Usoke, Rais Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Ndono-Urambo yenye kilomita 52 ambayo inaungana na Barabara ya Tabora-Ndono yenye kilomita 42 ambayo Rais Kikwete aliizindua jana kwenye siku ya tatu ya ziara yake.
Barabara hiyo iliyofanyiwa usanifu mwaka 2006 inajengwa na Kampuni ya CCECC ya Jamhuri ya Watu wa China kwa gharama ya Sh. Bilioni 59.764 na ujenzi wake utamalizika katika miezi 24 ijayo. Kampuni ya CCECC ndiyo ilijenga Reli ya TAZARA na Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria.
Baadaye, Rais Kikwete amezindua maabara ya masomo ya sayansi kwenye Shule ya Sekondari ya Kaliua High School, iliyoko nje kidogo ya mji wa Kaliua. Maabara hizo za fikizia, kemia na biolojia zimegharimiwa na ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Shule hiyo iliyofunguliwa mwaka 1997 kama shule ya sekondari ya wananchi na ikiwa na wanafunzi 80, sasa ina wanafunzi 1,102 ambako kati yao 695 ni kutwa na wa kidato cha kwanza hadi cha nne na wanafunzi 407 ni wa kidato cha tano na sita.
Mwaka 2007 ilianza kutoa masomo ya michepuo miwili ya sayansi kwa wanafunzi 40. Shule hiyo ambayo imekuwa shule ya kata sasa iko chini ya Serikali.