Rais Kikwete Aweka Jiwe la Msingi kwa Miradi ya Kihistoria Tabora

Barabara ya Tabora-Ndono yenye urefu wa kilomita 42 na inayojengwa na Kampuni ya Chico pia kutoka China kwa gharama ya Sh. Bilioni 51.34 na itamalizika katika kipindi cha miezi 20 kuanzia sasa. Gharama za mradi huo ni pamoja na Sh. Milioni 480 ambazo zimelipwa kwa wananchi kama fidia ya kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

JANA, Jumanne, Januari 8, 2013, imekuwa siku ya historia kwa Mkoa wa Tabora wakati maelfu ya wananchi wa Mkoa huo walipomshuhudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara kubwa tatu za lami ambazo baadhi yake zinaunganisha Mkoa huo na mikoa mingine na ambazo ujenzi wake unagharimu mabilioni ya fedha za wananchi.
Barabara kubwa hizo ni za Nzega-Tabora, Tabora-Ndono hadi Urambo, na Tabora hadi Nyahua ambazo ujenzi wake unakadiriwa kugharimu kiasi kinachokaribia Sh. Bilioni 350 ambazo zote zinatolewa na Serikali ya Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya siku tano ya Mkoa wa Tabora kujionea mwenyewe jitihada za wananchi kujiletea maendeleo, ameanza siku yake ya jana kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Nzega-Puge-Tabora yenye urefu wa kilomita 115 katika sherehe iliyofanyika kwenye eneo la Puge kilomita 58.2 kutoka mjini Nzega kuelekea Tabora.
Barabara hiyo ambayo usanifu wake ulifanyika mwaka 2009 imegawanywa katika sehemu mbili za Nzega-Puge na Puge-Tabora na itagharimu jumla ya Sh. Bilioni 135, zikiwamo fedha ambazo zimetumika kufidia wananchi ambao wanaathiriwa na ujenzi wa Barabara hiyo.
Sehemu ya Nzega-Puge inagharimu Sh. Bilioni 66.36, inajengwa na kampuni ya CCCC ya China na itakamilika katika katika miezi 27 ijayo. Sehemu ya Puge-Tabora yenye urefu wa kilomita 56.8 inajengwa kwa gharama ya Sh. Bilioni 62.74 na kampuni ya Sino Hydro ya China na itakuwa imekamilika katika miezi 26 ijayo.
Mradi mkubwa wa pili ambao Mheshimiwa Rais ameuwekea jiwe la msingi ni wa ujenzi wa Barabara ya Tabora-Ndono ambayo hata hivyo ujenzi wake utaendelezwa hadi kufikia mjini Urambo. Sherehe za uwekaji jiwe la msingi la Barabara hiyo iliyofanyiwa usanifu mwaka 2006 zimefanyika katika eneo la Mlolo, nje kidogo ya mji wa Tabora.
Barabara ya Tabora-Ndono yenye urefu wa kilomita 42 na inayojengwa na Kampuni ya Chico pia kutoka China kwa gharama ya Sh. Bilioni 51.34 na itamalizika katika kipindi cha miezi 20 kuanzia sasa. Gharama za mradi huo ni pamoja na Sh. Milioni 480 ambazo zimelipwa kwa wananchi kama fidia ya kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Barabara ya tatu kubwa ambayo Rais Kikwete ameiwekea jiwe la msingi ni ile ya Tabora hadi Nyahua yenye kilomita 85.6 na ambayo ujenzi wake unagharimu kiasi cha Sh. Bilioni 93.4.
Ujenzi wa barabara hiyo unakadiriwa kumalizika mwanzoni mwa mwaka ujao 2014 na inajengwa na Kampuni ya CFTEC pia kutoka Jamhuri ya Watu wa China na sherehe zake za uwekaji jiwe la msingi zimefanyika katika eneo la Cheyo B, nje kidogo ya Mji wa Tabora.
Kwa Rais Kikwete kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo tatu, katika miezi michache ijayo na kwa mara ya kwanza Mji wa Tabora utakuwa umeunganishwa kwa barabara za lami kutoka kaskazini (tokea Nzega) kutoka magharibi (kutokea Urambo) na kutokea kusini (tokea Nyahua).
Ujenzi wa Barabara ya Nzega-Tabora kwa lami una maana kuwa makao makuu ya Mkoa wa Tabora sasa yanaunganishwa na Mkoa wa Shinyanga, ujenzi wa Barabara ya Tabora-Nyahua unalenga kuunganisha kwa lami Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Dodoma wakati Barabara ya Tabora-Ndono hadi Urambo na hadi Kaliua unaenda kuunganisha kwa lami Mkoa wa Tabora na ule wa Kigoma.
Aidha, ujenzi wa Tabora-Nyahua na Tabora-Ndono hadi Urambo na hatimaye Kaliua unalenga kujenga kilomita 700 za lami kutoka Manyoni, Mkoa wa Dodoma hadi Kigoma. Novemba 5, mwaka jana, 2012, Rais Kikwete aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Manyoni-Itigi-Chaya yenye kilomita 89.
Barabara hizo zote pia zinajengwa kulingana na ahadi ya Mheshimiwa Kikwete wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kwa sababu ya ukosefu wa wafadhili wa kuchangia gharama za ujenzi wa barabara hizo, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania asilimia 100.