RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa maoni ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yatakuwa mchango mkubwa kuhusu nini kifanyike baada ya kumalizika kwa kipindi cha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG).
Aidha, Rais Kikwete ameipongeza nchi ya Sri Lanka kwa kuandaa vizuri na kwa mpangilio mzuri Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliomalizika, Novemba 17, 2013.
Rais Kikwete ameyasema hayo na kutoa pongezi hizo Novemba 16, 2013, wakati alipotoa Salamu za Shukurani kwa niaba ya viongozi wote waliohudhuria Mkutano huo kwenye Chakula cha Usiku rasmi kilichoandaliwa na Rais wa Sri Lanka, Mahinda Rajapaksa kwenye Ikulu ya Temple Trees ya nchi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wenzake, Rais Kikwete amesema: “Mada ya mwaka huu ya mkutano wetu wa CHOGM ya Maendeleo ya Pamoja kupitia Ukuaji wa Pamoja imekuja kwa wakati unaofaa. Kwa taasisi kama ya kwetu ambayo inawakilisha watu bilioni mbili kujadili suala hilo hasa kwa kutilia maanani mjadala unaoendelea kuhusu ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 ni jambo la busara sana.”
Mkutano wa CHOGM ambao ulianza juzi, Ijumaa, Novemba 15, 2013, umemalizika leo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kumbukumbu ya Bandaranaike mjini Colombo, Sri Lanka.
Akizungumzia mkutano huo, Rais Kikwete amesema: “Tunakupongeza Mheshimiwa Rais kwa maandalizi mazuri ya Mkutano huo. Tunajua siyo kazi rahisi kuandaa Mkutano wa ukubwa huu. Lakini kwa uongozi wako wa busara na uongozi wako, kwa kusaidiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, kila kitu kimekwenda vizuri.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kwa niaba ya viongozi wenzangu waliokusanyika hapa jioni ya leo, napenda kukutakia wewe, Mheshimiwa Rais, kila la heri katika uendeshaji wa taasisi yetu hii.”