RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wabia wa maendeleo wa nchi masikini kutimiza ahadi zao kama njia ya uhakika kuhakikisha Malengo ya Milenia yanayolenga kuzitoa nchi masikini kwenye uduni na kuziharakishia maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania itaweza kutekeleza kwa ukamilifu baadhi ya Malengo lakini itakuwa vigumu kutelekeza Malengo yote manane kama inavyotakiwa chini ya Makubaliano ya Utekelezaji wa Malengo ya Milenia hayo ifikapo mwaka 2015.
Rais Kikwete ameyasema hayo Septemba 24, 2013 wakati alipozungumza kwenye mkutano uliojadili Jinsi Gani ya Kuongeza Kasi ya Utekelezaji wa Malengo ya Milenia ulioandaliwa na Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na Benki ya Dunia (WB) na uliofanyika kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Pamoja na Rais Kikwete kuzungumzia maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia katika nchi mbali mbali walikuwa na Mtawala wa UNDP, Hellen Clark, Rais wa Benki ya Dunia, Jim Kim, Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina, Rais wa Ghana, John Mahama, Rais wa Costa Rica Laura Chinchilla Miranda na Waziri Mkuu wa Tonga, Lord Siale’ataongo Tu’ivakano.
Katika kikao ambacho kila mmoja wa viongozi hao alitoa uzoefu na changamoto za nchi yake katika kutekeleza Malengo hayo, Rais Kikwete amewaambia wafadhili kuwa wakati nchi zinaendelea na utekelezaji wa Malengo hayo, ni wajibu wa wafadhili pia kutimiza wajibu wao wa Lengo la Nane la Milenia ambalo linawabebesha wajibu wafadhili kugharimia utekelezaji wa Malengo hayo.
Rais Kikwete amesema kuwa kukawia kwa wafadhili hao kutoa fedha za utekelezaji wa Malengo, zimechangia kwa kiasi fulani kwa utekelezaji huo kutokuwa na kasi iliyotarajiwa kutokea mwanzo.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na kucheleweshwa kwa fedha za kutosha za utekelezaji, Tanzania itaweza kwa kiasi fulani kufanikisha utekelezaji wa baadhi ya Malengo, lakini ni dhahiri kuwa Malengo mengine hayataweza kufikiwa ifikapo mwaka 2015 ambao ndiyo mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Malengo hayo.
“Tunafanya juhudi kubwa na ni dhahiri kuwa kasi ya jitihada hizo itaongezeka katika miaka miwili iliyobakia. Kwa jumla ripoti ya utekelezaji wa Malengo hayo katika Tanzania inaonyesha kuwa ni dhahiri haitawezekana kutekeleza Malengo matatu ambayo ni Lengo la Kwanza la Kufuta Umasikini wa Kutupwa na Njaa, Lengo la Tano la Kuinua Kiwango cha Afya na Kupunguza Vifo vya Akinamama, na Lengo la Saba la Kuhakikisha Tanzania Inakuwa na Mazingira Endelevu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Malengo ambayo Tanzania itayafikia bila matatizo ni pamoja na Lengo la Pili la Kuhakikisha kuwa Watoto Wote Wenye Umri wa Kwenda Shule Wanakwenda Shule, Lengo la Nne la Kupunguza Vifo vya Watoto, Lengo la Sita la Kupunguza Ukali wa Magonjwa ya Malaria na Ukimwi na Sehemu ya Lengo la Saba Kuhusu Uongezaji wa Idadi ya Watu Wanaopata Maji safi na Salama ya Kunywa.”
“Tunaweza pia kufikia Lengo la Tatu la Kufanikisha Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Akinamama hasa katika kuhakikisha kuwa idadi sawa ya watoto wa kike na kiume wanakwenda shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu na kuwa na idadi sawa ya wanawake na wanaume katika Bunge,” amesema Rais Kikwete.
Malengo ya Milenia yamekuwa yanatekelezwa tokea mwaka 2001 na yalenga kuzitoa nchi masikini katika umasikini na uduni na kuzifungulia njia ya maendeleo.