Rais Kikwete Awataka Viongozi Tanga Kusimamia Watoto Shule

Mrisho Gambo

Mrisho Gambo

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule, wana kwenda shule bila kukosa hata kama hawana uwezo wa kumudu mahitaji maalum ya shule. Rais amesema hayo Wilayani Korogwe wakati akipokea taarifa ya Wilaya iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Bw. Mrisho Gambo.

Katika taarifa yake kwa Rais, Bw. Gambo ameelezea hali ya mdondoko wa wanafunzi Wilayani mwake na kuelezea kuwa unasababishwa na utoro, mimba, vifo na wazazi kukosa mahitaji muhimu kwa watoto wao.

Ndipo Rais Kikwete akasema kuwa “Ni lazima warudi shule ni, na viongozi mtafute namna ya kuwasaidia, msiwaache bure, muwatafutie na muwapatie hayo mahitaji maalum wanayotakiwa kuwa nayo” Rais amesema na kusikitishwa na taarifa hizo ambazo amewaagiza viongozi wa Wilaya kuwatafuta watoto hao walipo na wale wasio na mahitaji maalum ambayo baadhi yake ni sare za shule, kuhakikisha kuwa uongozi wa Halmashauri husika zinawatimizia hayo mahitaji na kuwapa watoto fursa ya kuwa shuleni.

Taarifa za Wilaya zinaonesha kuwa Mwaka 2011 jumla ya watoto 63,918 waliandikishwa shule na Kati yao watoto 492 hawakuhudhuria shule kwa sababu mbalimbali. Rais pia amezitaka Wilaya kuweka mkakati wa kutengeneza madawati kwa ajili ya shule zao, kuwa na nyumba za walimu, ujenzi wa madarasa, maabara na vitabu. Rais Kikwete yuko Mkoani Tanga kwa ajili ya shughuli za kikazi na kukagua miradi ya maendeleo, kuangalia utekelezaji wa ahadi na Ilani ya Chama.

Mara baada ya kuwasili Mkoani Tanga siku ya Jumapili tarehe 23 Machi, 2014, Rais ameweka jiwe la Msingi la ujenzi wa bwawa la Maji, Mkata Wilayani Handeni na kuzindua ujenzi wa barabara ya Handeni-Korogwe na Handeni-Mkata ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama za serikali kwa asilimia Mia moja.

Katika siku yake ya pili katika Wilaya ya Korogwe, pamoja na mambo mengine Rais amezindua barabara ya Korogwe – Mumbara na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Maabara ya shule ya Sekondari Madago kabla hajahutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Mombo. Ziara ya Rais Mkoani Tanga itakuwa kwa awamu mbili ambapo awamu hii ya kwanza atatembelea Wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga Mjini na awamu ya pili itahusisha Wilaya za Kilindi, Lushoto, Mkinga na Pangani.