Na Joachim Mushi
RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda kundi la UKAWA waliogoma kuendelea na majadiliano ya kuandaa katiba mpya katika bunge la katiba kurudi bungeni na kuendelea na majadiliano.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam katika viwanja vya sabasaba alipokuwa akilihutubia taifa kwa kuzungumza na vijana na kupokea maandamano ya kizalendo yaliyofanywa na vijana. Akizungumza na umati huo wa vijana alisema nafasi waliopewa wajumbe wa katiba ni ya kipekee hivyo kitendo cha baadhi ya wajumbe hao kugoma kuendelea na majadiliano ya kuunda katiba mpya ni kuwakosea wananchi wanaowawakilisha.
Alisema njia pekee ya wabunge wa katiba ni kutumia vema fursa hii walionayo kuhakikisha wanatutengenezea katiba nzuri. Katiba ambayo itaondoa matatizo yaliyojitokeza katika muungano yanayohitaji kurekebishwa na katiba mpya. “…Ndugu wananchi lazima nikiri kuwa binafsi sikufurahishwa hata kidogo na kitendo cha baadhi ya wajumbe wa bunge hilo kususia vikao vya bunge…nimesikitika sana eti hata wameamua kuzunguka nchi kwenda kushtaki kwa wananchi sijui wanakwenda kumshtaki nani na kuhusu jambo gani, napenda kujumuika na baadhi ya watu wema na kuwasii warudi bungeni na kuendelea na mchakato wa kutunga katiba,” alisema.
Alisema muda wa kwenda kwa wananchi bado haujafika na ukifika wakati huo wajumbe wote wataruhusiwa kwenda kuwaelimisha wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashawishi ili wakubaliane na katiba hiyo iliyopitisha kabla ya kuipigia kura za ndiyo kuiunga mkono katiba hiyo kutumika. Alisema kitendo cha wabunge hao kutoka nje ya bunge kinawaba baadhi ya watu kuwashuku kwamba labda huenda hawana nia njema na jambo jema linalofanyika kwa sasa.
Aidha aliwataka wajumbe wote wa katiba kuacha lugha za matusi na kujadili mada iliyopo mbele yao kwani kutumia lugha hiyo ndio chanzo ya mvutano kwa wajumbe. “…Najua kinachowasumbua wajumbe wote ni uhusiano miongoni mwao na tatizo hili majibu yao wanayowenyewe kati ya kambi moja na nyingine, tatizo kubwa la wajumbe hawa ni kutumia lugha isiyo na staha pande zote za wajumbe.
Alisema kila upande wa wajumbe unamchango wake kupitia umoja wao hivyo hawana budi kuvumiliana na kusikilizana na hatimaye kutoka kwa kukubaliana pasipo kuchukiana jambo ambalo linataka kuwashinda baadhi ya wajumbe. “…Unamkuta mbunge na heshima zake akitoa matusi yanayokaribia ya nguoni…mimi nilisema mjumbe hana haja ya kutumia lugha ya matusi kwa mjumbe mwenzake kwa kujenga hoja yake, we sema tu kwanini inafaa au kwanini haifai…lakini unakuta mtu anamtukana na aliyetoa hoja ndipo unaendelea,” alisema Raid Kikwete akilihutubia taifa kupitia vijana.
Alisema inahudhunisha zaidi baada ya baadhi ya wajumbe kuwatukana waasisi wa taifa letu, jambo ambalo alisema haliwezi kuvumilika. Alisema wanaofanya hivyo hawatumii vizuri uhuru wao wa kutoa mawazo. “…Hivi huo ndio uhuru wa kutoa mawazo? Ndugu zangu hawa ni mashujaa wetu…walijitolea maisha yao kwa ajili ya kulikomboa taifa…,” alisisitiza Rais Kikwete. Alibainisha kuwa mwalimu Julias Nyerere aliamua kuacha kazi ya mshahara na kwenda kuongoza mapambano ya kudai uhuru jambo ambalo liliwashangaza watu wengi hivyo michango ya mashujaa kama hao hauwezi kubezwa hata kidogo.