Rais Kikwete Awasilisha Rambirambi za Watanzania kwa rais wa Nigeria

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Goodluck Jonatahn wa Nigeria jijini Abuja leo May 8, 2014 pembeni ya Mkutano wa Dunia wa Uchumi. PICHA NA IKULU.

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Goodluck Jonatahn wa Nigeria jijini Abuja leo May 8, 2014 pembeni ya Mkutano wa Dunia wa Uchumi. PICHA NA IKULU.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Mei 8, 2014, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan katika Hoteli ya Transcorp Hilton katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Abuja. Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete kwa mara nyingine, amewasilisha rambirambi rasmi za Tanzania, za Watanzania na za kwake mwenyewe kwa kiongozi huyo wa Nigeria kufuatia vitendo vya kigaidi ambavyo vimeua maelfu ya watu na wengine kutekwa nyara katika maeneo mbali ya nchi hiyo na hasa kaskazini.

Rais Kikwete pia ametoa pongezi nyingi kwa Rais Jonathan na wananchi wa Nigeria kwa kuandaa Kongamano la Uchumi Duniani (WEF-Afrika) kwa Afrika lenye mafanikio makubwa. Kongamano hilo lilianza jana na linamalizika kesho mjini Abuja na Rais Kikwete amejiunga na viongozi kadhaa duniani kuhudhuria Kongamano hilo.

“Mheshimiwa Rais, nakushukuru sana kwa kupata muda wa kuja kujiunga nasi katika mkutano wetu huu mkubwa. Kama ulivyosema wewe mwenyewe kuwepo kwako na kwa viongozi wengine ni ishara muhimu kwa dunia kuwa nchi yetu, pamoja na matatizo makubwa ambayo tunapitia, bado inaungwa mkono duniani na ina usalama wa kutosha kuweza kuendesha mkutano kama huu,” Rais Jonathan amemwambia Rais Kikwete.

Naye Rais Kikwete amemwambia Rais Jonathan: “Tunakupogeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuandaa kongamano zuri hapa nchini kwako. Kama unavyojua miaka yote makongamano hayo yalikuwa yanafanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini, mpaka sisi Tanzania tulipoandaa Kongamano la kwanza nje ya Afrika Kusini. Siyo kazi rahisi, tunakupongeza sana.”
“Na yale yanayoendelea katika nchi ni uendawazimu wa kiwango cha juu sana – binadamu anao uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo ya ukatili wa hatari kabisa. Hawa ni watu wasio na roho wala moyo. Ni ukatili wa kiwango cha juu sana,” amesema Rais Kikwete.

Hata hivyo, Rais Jonathan ameonyesha matumaini kuwa ugaidi huo unaweza kuwa unaelekea mwisho hasa kufuatia uamuzi wa Marekani na Uingereza kuisaidia Nigeria kukabiliana na hali hiyo. Ufaransa na China pia zimejitolea kusaidiai.
Moja ya mambo yanayoiwekea shinikizo Serikali ya Rais Jonathan kwa sasa ni kutekwa nyara kwa watoto wa kike wa Sekondari zaidi ya 200 katika shule moja kaskazini mwa nchi hiyo zaidi ya wiki tatu zilizopita. Mpaka sasa hawajulikana walipo na kikundi cha Boko Haram ambacho kinapinga elimu ya magharibi kimesema kinawashikilia watoto hao na kinataka kuwauza kwenye utumwa.
Juzi, Kikundi hicho ambacho kinafanya kila aina ya ugaidi kiliteka nyara watu wengine wanane kutoka kijiji kimoja cha kaskazini mwa nchi hiyo na usiku wa jana, kikundi hiki kilivamia vijiji kadhaa na kuua watu zaidi ya 300.

Wakati huo huo; Katika salamu zake za pole kwa Rais Jonathan, Rais Kikwete amesema: “Napenda kutoa salamu za rambirambi na pole zetu nyingi kwako Mheshimiwa Rais na wananchi wa Nigeria kufuatia mfululizo wa vitendo vya kigaidi ambavyo vimepoteza maisha ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo na wengine kutekwa nyara. Tumekuja kuonyesha mshikamano wetu na wananchi wa Nigeria.”

Rais Kikwete ametoa pole hizo mwanzoni mwa hotuba yake kwenye mkutano wa marais uliozungumzia umuhimu wa miundombinu ya kimkakati katika Afrika ikiwa ni sehemu ya Kongamano la Uchumi Duniani (WEF) Afrika kwenye Hoteli ya Transcorp Hilton mjini Abuja, Nigeria.

“Tulishauriwa sana tusije kuhudhuria kongamano hili kwa sababu ya hali ya usalama. Lakini tusingefika tungewapa ushindi magaidi hawa ambao wanasumbua sehemu kubwa ya Bara letu. Mheshimiwa Rais sala zetu ziko nawe na wananchi wa Nigeria katika kipindi hiki kigumu.”

Serikali ya Nigeria imekuwa inapambana na vikundi vya kigaidi na hasa kile cha Boko Haram ambacho kimekuwa kinaendesha kila aina ya ugaidi hasa katika maeneo ya kaskazini ya nchi hiyo. Wiki tatu zilizopita, kikundi hicho ambacho lengo lake kuu ni kupinga elimu ya magharibi kiliteka watoto zaidi ya 200 wa kike kutoka mabweni ya shule moja ya sekondari kaskazini mwa nchi hiyo. Mpaka sasa watoto hao hawajapatikana, jambo ambalo linaipa shinikizo kubwa Serikali ya Nigeria. Boko Haram kimetishia kuwauza sokoni watoto hao wa kike. Siku mbili zilizopta, kikundi hicho kiliteka nyara watu wengine wanane na usiku wa jana, kimeua watu wanaokadiriwa kufikia 300 katika vijiji mbali mbali vya eneo la kaskazini mwa nchi hiyo.