Rais Kikwete Awasili Uswisi, Aanza Vikao vya Kazi

Rais Dk.Jakaya Mrisho Kikwete akikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan mjini Geneva.

Rais Dk.Jakaya Mrisho Kikwete akikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan mjini Geneva.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa linalochunguza jinsi dunia inavyoweza kujikinga na majanga ya magonjwa ya mlipuko katika miaka ijayo, Jakaya Kikwete, aliwasili mjini Geneva, Uswisi, Julai 14, 2015, kwa ajili ya kuendesha vikao vya Jopo hilo.
Vikao hivyo vitakuwa ni awamu ya pili kwa Jopo hilo ambalo liliteuliwa Aprili, mwaka huu, 2015 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon.
Wajibu mkuu wa Jopo hilo ni kutoa mapendekezo ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa, ili kuweza kuzuia ama kudhibiti kwa uhakika zaidi majanga ya magonjwa ya mlipuko kufuatia balaa la Ebola katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea ambalo limeua maelfu kwa maelfu ya watu.
Jopo hilo lilifanya vikao vyake kwa mara ya kwanza Mei, mwaka huu, katika makao makuu ya UN mjini New York, Marekani. Vikao vya sasa vilivyoanza juzi, Jumatatu, Julai 13, 2015 vitachukua siku tano na vitafanyika kwenye Ofisi za UN na zile za Shirika la Umoja wa Mataifa ya Afya (WHO) mjini Geneva.
Mbali na Mwenyekiti Rais Kikwete, wajumbe wengine wa Jopo hilo ni Bwana Celso Amorim wa Brazil na aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi yake, Bi. Micheline Calmy-Rey ambaye ni Rais wa zamani wa Shirikisho la Uswisi, Narty Natalegawa ambaye alipata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Dr. Joy Phamaphi ambaye ni Katibu Mtendaji wa Umoja wa Viongozi wa Afrika katika Mapambano dhidi ya Malaria (ALMA) na waziri wa zamani wa afya wa Botswana na Dr. Rajiv Shah ambaye mpaka majuzi alikuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Marekani (USAID).
Hata hivyo, vikao vya sasa vitahudhuriwa na wajumbe wanne badala ya sita. Bwana Shaha atafuatilia vikao vya sasa kwa njia ya mkutanomtandao (tele-conference) na Bwana Natalegawa aliondoka mjini Geneva jana usiku kurejea nyumbani kuwahi sikukuu ya Idd El Fitri.