RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Warsaw, Poland, asubuhi ya Novemba 19, 2013, kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi ambako analiwakilisha Bara la Afrika.
Rais Kikwete amewasili Poland akitokea Dubai, alikosimama kwa muda akiwa njiani akitokea Colombo, Sri Lanka, ambako aliungana na viongozi wengine wa Jumuiya ya Madola kushiriki Mkutano wa Viongozi wa Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo uliomalizika mwishoni mwa wiki.
Kwenye Mkutano huo wa Mabadiliko ya Tabia Nchi unaojulikana kama Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Tabia Nchi -Conference of Parties on the Convention na Mkutano wa Tisa wa Nchi Wanachama wa Itifaki ya Kyoto – Meeting of the Parties of the Kyoto Protocal – COP 19/CMP -9, Rais Kikwete anawasilisha Bara la Afrika.
Rais Kikwete ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Marais wa Afrika kuhusu Tabia Nchi (CAHOSCC) ambayo ndiyo inatoa msimamo na mwelekeo wa kisiasa wa Bara la Afrika kuhusu masuala ya Tabia Nchi.
Rais Kikwete alichaguliwa na wenzake kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo wakati wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Addis Ababa, Ethiopia, mwanzoni mwa mwaka huu. Rais Kikwete alichukua nafasi ya Hayati Meles Zenawi wa Ethiopia ambaye alifariki dunia Septemba mwaka jana, 2012.
Mkutano huo wa COP19/CMP-9 unafunguliwa mchana wa leo kwenye Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Warsaw na Rais Kikwete ni mmoja wa viongozi wanaozungumza kwenye ufunguzi huo.
Wengine ambao wanazungumza kwenye ufunguzi huo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon, Waziri Mkuu wa Poland Mheshimiwa Donald Tusk na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu, Mheshimiwa Balozi William Ashe.
Kwenye Hoteli ya Bristol mjini Warsaw, Rais Kikwete amepokelewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Mheshimiwa Theresia Huvisa ambaye amekuwa anaongoza ujumbe wa awali wa Tanzania katika vikao vya maandalizi ya COP-19-CMP 20.
Mara baada ya kuwasili hotelini, Rais Kikwete amepewa maelekezo kuhusu Mkutano huo na Waziri Huvisa na baadaye kupewa maelezo na ujumbe wa AU ukiongozwa na Mheshimiwa Rhoda Tumusiime, Kamishna wa AU na Bwana Emmanuel Dlamini, Mwenyekiti wa Wataalam wa Majadiliano wa Kundi la Afrika.
Wakati huo huo: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, ameushukuru Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund for Development) kwa kuonyesha matumaini ya kugharamia ujenzi wa barabara ya Uvinza-Malagarasi yenye urefu wa kilomita 51 kwa kiwango cha lami, kwa gharama ya shilingi bilioni 31.869.
Aidha, Rais Kikwete pia ameushukuru Mfuko huo kwa kugharamia ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Uvinza yenye urefu wa kilomita 76.6 kwa kiwango cha lami, ujenzi ambao umekamilika kwa asilimia 100, kwa gharama ya Shilingi bilioni 78.241.
Mfuko huo tayari umeonyesha matumaini ya kukubali maombi ya Serikali ya fedha za ujenzi wa barabara hiyo ya Uvinza-Malagarasi yalilowasilishwa mwezi Machi mwaka huu. Kilichobaki sasa ni bodi ya mfuko huo kuidhinisha mpango huo wa maendeleo ya miundombinu katika siku chache zijazo.
Rais Kikwete ametoa shukurani hizo alipokutana na Mrithi wa Kiti cha Ufalme cha Abu Dhabi ambaye pia ni Naibu Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ya Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Mohamed bin Zayed bin Sultan al Nahyan, leo, Jumatatu, Novemba 18, 2013, mjini Abu Dhabi. Rais Kikwete ameonana na Mrithi huo wakati aliposimama kwa muda Dubai akitokea Colombo, Sri Lanka, alikohudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Rais Kikwete ambaye pia alikutana na kutoa shukurani zake kwa Mkurugenzi Mkuu wa Abu Dhabi Fund for Development Bw. Mohamed Saif Al Suwaidi, ameelezea furaha yake kwa kuwapo na matumaini ya kupatikana kwa fedha hizo, amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza kasi za juhudi za Serikali za kuunganisha kwa lami mkoa wa Kigoma na Dar es salaam ndani ya miaka miwili ama mitatu ijayo.
Hivi sasa tayari Serikali ya Korea inagharamia ujenzi wa Barabara ya Kigoma-Kidahwe yenye urefu wa kilomita 48.
Rais Kikwete amesema: “Nafarijika sana kwa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kuonyesha matumaini ya kugharamia ujenzi wa barabara ya Uvinza-Malagalasi. Mfuko umekubali ombi letu la fedha kilichobaki ni Bodi yake kuuridhia katika siku chache zijazo.”
“Ujenzi wa barabara hiyo ya Uvinza-Malagarasi ukikamilika pamoja na ule wa ujenzi wa barabara ya Tabora-Urambo, Tabora-Nyahuwa, pamoja na ujenzi wa barabara ya Manyoni-Chanya unaogharamiwa na serikali ya Korea Kusini, kilomita zipatazo 200, zitakuwa zimejengwa na usafiri kutoka Kigoma hadi Dar es salaam utakuwa katika barabara ya lami.
Rais Kikwete, ambaye yuko njiani kuelekea Warsaw, Poland, kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya Mabadiliko ya hali ya hewa duniani, alipata nafasi pia kushuhudia maonyesho ya mwaka huu ya Dubai Airshow 2013 katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Al Maktoum eneo la Dubai World Central.
Maonyesho hayo, ambayo ni ya tatu kwa ukubwa duniani, yanashirikisha zaidi ya makampuni 1000 kutoka sehemu mbalimbali yakihusisha kila aina ya ndege za kivita, za abiria, za mizigo na za michezo.