Rais Kikwete Awasili Canada kwa Ziara ya Kiserikali

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua gwaride rasmi katika viwanja vya jumba la Rideau Hall jijini Ottawa, Canada, katika hatua yake ya kwanza ya ziara rasmi ya siku mbili jijini humo Jumatano Oktoba 4, 2012. Jumba hilo ndilo makazi na ofisi rasmi ya Gavana Jenerali wa Canada tangia mwaka 1867 ambapo pamoja na kuishi humo pia hapo ndipo hutumika kwa kuwatunukia wananchi wa Canada waliofanya vyema, pa kupokelea wageni mashuhuri wa nchi za nje na pia ndipo anapofanyia shughuli zote za kitaifa akiwa kama mwakilishi wa Malkia wa Uingereza. Picha na Ikulu.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika viwanja vya jumba la Rideau Hall jijini Ottawa, Canada, katika hatua yake ya kwanza ya kuanza ziara rasmi ya siku mbili jijini humo Jumatano Oktoba 4, 2012. Jumba hilo ndilo makazi na ofisi rasmi ya Gavana Jenerali wa Canada tangia mwaka 1867 ambapo pamoja na kuishi humo pia hapo ndipo hutumika kwa kuwatunukia wananchi wa Canada waliofanya vyema, pa kupokelea wageni mashuhuri wa nchi za nje na pia ndipo anapofanyia shughuli zote za kitaifa akiwa kama mwakilishi wa Malkia wa Uingereza.


Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wake katika mazungumzo na Gavana Jenerali wa Canada Mhe. David Johnson na mkewe Mama Sharon Johnson na viongozi wa serikali ya nchi hiyo katika jumba la Rideau jijini Ottawa, Canada, katika hatua yake ya kwanza ya ziara rasmi ya siku mbili jijini humo Jumatano Oktoba 4, 2012. Picha na Ikulu.


Na Mwandishi Maalumu, Ottawa, Canada

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewasili mjini Ottawa, Canada, mchana wa Oktoba 3, 2012, kuanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika nchi hiyo kwa mwaliko wa Gavana Jenerali, David Johnston.
Rais Kikwete na ujumbe wake wamewasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Macdonald-Cartier wa mji mkuu wa Canada wa Ottawa kiasi cha saa nane na dakika 55 mchana baada ya safari ya ndege ya saa moja kutoka mjini New York, Marekani, ambako amefanya ziara ya siku mbili pia.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Ottawa, Rais Kikwete amelakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, John Baird, Balozi wa Tanzania katika Canada, Alex Masinda, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada, Deepak Obhrai, Balozi wa Canada katika Tanzania, Robert Orr na Mbunge Joe Daniel.
Miongoni mwa viongozi wengine walimpokea Rais kwenye Uwanja wa Ndege huo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe na Waziri wa Nishati na Madini, Sospter Muhongo ambao wametangulia kuja Canada lakini ni sehemu ya ujumbe wa Rais Kikwete kwenye ziara hiyo.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wake katika mazungumzo na Gavana Jenerali wa Canada Mhe. David Johnson na mkewe Mama Sharon Johnson na viongozi wa serikali ya nchi hiyo katika jumba la Rideau jijini Ottawa, Canada, katika hatua yake ya kwanza ya ziara rasmi ya siku mbili jijini humo Jumatano Oktoba 4, 2012


Kwenye Uwanja wa Ndege huo, Rais Kikwete pia ameweka saini kwenye kitabu cha kumkaribisha rasmi Canada. Kutoka uwanja wa ndege, msafara wa Rais Kikwete umekwenda moja kwa moja hadi kwenye Nyumba ya Serikali, ambako Kikwete ametoka kwenye gari na kuingia kwenye gari maalum linalovutwa kwa farasi na kuelekea kwenye Viwanja vya Jumba la Rideau ambako amepokelewa rasmi, kwa mbwembwe zote za Ziara Rasmi ya Kiserikali.
Mara baada ya kuwasili kwenye Viwanja vya Jumba la Rideau, Rais amepokelewa na Gavana Jenerali Johnston na mkewe, Mama Sharon Johnston, amepewa heshima ya kupigiwa mizinga 21 na pia amekagua Gwaride la Heshima la Majeshi ya Ulinzi ya Canada.
Katika hotuba fupi kwenye sherehe hiyo ya mapokezi ambayo pia imehudhuriwa na Watanzania wanaoishi Canada, Rais Kikwete ameishukuru Canada kwa misaada mingi ya maendeleo ambayo imechangia sana katika jitihada za Tanzania kujiletea maendeleo tokea uhuru mwaka 1961.
Akizungumza wakati akimkaribisha Kikwete, Gavana Jenerali amemshukuru Rais Kikwete kwa kukubali kufanya ziara hiyo ambayo iliahirishwa mapema mwaka huu kutokana na ajali ya meli M.V. Skargit iliyozama kwenye pwani ya Zanzibar na kupoteza maisha ya watu.
Amesema Gavana Jenerali Johnston: “Nafurahi sana umeweza kupata muda wa kuja kututembelea Mheshimiwa Rais na ninayo heshima sana kukukaribisha kwenye Jumba la Rideau, nyumbani kwa wananchi wa Canada.”
Ameongeza: “Tumekuwa na uhusiano mzuri kwa miaka mingi na kwa hakika hizi ni nyakati za kusisimua na zenye changamoto nyingi kwa nchi zetu mbili ambazo zinaendelea kujenga jamii zenye uvumilivu na za kidemokrasia.”
Mara baada ya sherehe za mapokezi, Kikwete na mwenyeji wake wamefanya mazungumzo ya kiasi cha dakika 40 kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuhusu masuala ya kimataifa. Usiku wa Oktoba 3, 2012 Gavana Jenerali Johnston ameandaa dhifa ya kitaifa kwa heshima ya Rais Kikwete kwenye Jumba la Rideau.