Rais Kikwete Awashangaa Viongozi Wenzake…!

Rais Kikwete kulia katika shughuli na viongozi wengine.

Rais Kikwete kulia katika shughuli na viongozi wengine.

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akifunua kitambaa katika jiwe la msingi wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Kibaha. Kushoto ni Mbunge wa Kibaha mjini, Sylvestry Koka.

Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akifunua kitambaa katika jiwe la msingi wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Kibaha. Kushoto ni Mbunge wa Kibaha mjini, Sylvestry Koka.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema ni jambo la kushangaza kwamba baadhi ya viongozi wanashindwa kuwahamasisha na kuwahimiza wananchi kushiriki vizuri hata kilimo cha mboga.
Aidha, Rais Kikwete ametaka viongozi nchini kuendelea kusimamia vizuri miliki ya ardhi akisema kuwa baadhi ya walanguzi wanashikilia maeneo makubwa ya ardhi bila kuiendeleza na kuyatumia kukopea fedha katika mabenki ambazo wanazitumia kuendeleza maeneo mengine na siyo Kibaha. Pia, Rais Kikwete ametaka viongozi kuacha kukwamisha maendeleo ya wananchi kwa nia tu ya kila kiongozi kutaka kujenga himaya yake.

Akipokea taarifa ya maendeleo ya Wilaya ya Kibaha Oktoba 8, 2013, akiwa kwenye siku ya tano ya ziara ya kikazi kukagua na kuzindua shughuli za maendeleo katika Mkoa wa Pwani, Rais Kikwete ameshangazwa na kushindwa kwa viongozi wa Mkoa huo kuwahimiza wananchi kulima mboga kwenye Bonde la Ruvu.
“Hivi mnashindwa vipi, nyie viongozi wenzangu, kuwahimiza wananchi wenu kulima hata nyanya na mboga nyingine katika Bonde la Ruvu?”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nyanya zinatoka mbali huko, zinatoka Matombo, zinatoka Muheza, zinatoka hata Mpwapwa lakini nyie mnashindwa kuwahimiza wananchi wenu kushiriki kilimo cha mazao hayo katika Bonde la Ruvu? Mnashindwa vipi kuchukua hatua za kunufaika na soko kubwa la chakula la Jiji la Dar Es Salaam na nyie mko jirani tu?”
Hata hivyo, Rais Kikwete ameongeza, “mnashindwa kuwahamasisha wananchi lakini nyie wenyewe viongozi mna mashamba yetu ya nyanya.”
Amesema kuwa alipotembelea Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa ya Mkongo, Wilaya ya Rufiji wakati wa ziara yake ya sasa, alionyeshwa mfumo wa kilimo cha nyanya ambako aliambiwa kuwa miche 160 ilikuwa inazalisha kiasi kilo 50 kila mche na kuingiza kiasi cha Sh. milioni 13 kwa mwezi.
“Nyanya na mboga ni biashara kubwa sana na inaweza kuwatoa vijana wetu katika umasikini na eneo tunalo. Kama lipo tatizo la kiufundi na udongo wa eneo hilo kwa kilimo cha nyanya na mboga ipo pia namna ya kukabiliana na tatizo hilo.”
Kuhusu miliki ya ardhi katika Wilaya ya Kibaha, Rais amerudia wito wake wa kuwataka viongozi kusimamia miliki nzuri ya ardhi hiyo akifafanua kuwa ardhi ni msingi mkuu wa maendeleo ya wananchi.
“Najua pia wako watu ambao wanakuja hapa wanamilikishwa maeneo makubwa ya ardhi. Lakini wanachofanya ni kutokuyaendeleza maeneo hayo na badala yake wanatumia hati za kumiliki maeneo hayo kukopea fedha katika mabenki ambazo wanazitumia kuendeleza maeneo mengine na siyo Wilaya ya Kibaha ama Mkoa wa Pwani. Hii siyo barabara.”
Rais pia amesema kuwa ni muhimu kwa viongozi kuachana na tabia ya kujenga himaya katika shughuli za umma na badala yake washughulike na maendeleo ya kwelikweli ya wananchi.

Rais Kikwete ametoa kauli hiyo kutokana na mgongano wa mawazo baina ya viongozi wa Mkoa na Wilaya kuhusu hadhi ya Hospitali ya Shirika la Elimu Kibaha, baadhi wakidai kuwa hospitali hiyo ni ya shirika na hivyo kazi yake ni kuhudumia wafanyakazi wa shirika hilo tu na wengine wakisema ni hospitali ya Mkoa wa Pwani.
Rais Kikwete amesema kuwa hospitali hiyo ni mali ya Shirika la Elimu Kibaha lakini kwa sababu Shirika hilo ni mali ya Serikali basi hospitali hiyo ni mali ya Serikali na hivyo ni kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa Mkoa wa Pwani. “Ni hospitali ya Mkoa wa Pwani na lazima iendelezwa kwa dhana hiyo,”

Wakati huo huo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kikwete Oktoba 8, 2013, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi wa Mbu katika eneo la viwanda cha TAMCO la Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani. Kiwanda hicho kinachojengwa na Serikali ya Tanzania kwa raslimali zake yenyewe kinatumia teknolojia ya Wacuba na kitatengeneza dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu ambayo itawekwa katika maeneo ya mazalia ya mbu ikiwa ni jitihada za Serikali za kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria nchini.
Kiwanda hicho ambacho ujenzi wake unakaribia kukamilika ni cha kwanza na pekee katika Afrika.

Makubaliano ya kujengwa kwa kiwanda hicho ambacho kwa lugha ya kitaalam kinajulikana kama Biolarvicide Plant yalifikiwa mwaka 2009 wakati Rais Kikwete alipofanya ziara rasmi nchini Cuba na kutembelea Kiwanda cha LabioFarm ambacho ndicho chenye utaalam wa kutengeneza dawa hiyo. Kiwanda hicho kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni sita ya dawa ya mbu pia kina uwezo wa kuzalisha mbolea ya asili, chanjo ya binadamu na wanyama, dawa za wadudu wengine na vyakula vya watu wenye mahitaji maalum ya chakula. Aidha, kiwanda hicho kinatumia teknolojia rafiki kwa mazingira – Green Company.

Kiwanda hicho ambacho kinajengwa kwa gharama ya dola za marekani milioni 22 na Sh. bilioni tano za Tanzania kitaweza kuajiri wafanyakazi 170 na bidhaa zake zitauzwa ndani na nje ya Tanzania. Chini ya mipango ya ujenzi wa kiwanda hicho ambao kwa sababu mbali mbali umecheleweshwa kwa miezi 14 pamoja na kujengwa na Serikali ya Tanzania lakini kitatumia teknolojia ya Cuba ikiwa ni pamoja na ujenzi, ufundi, mafunzo na mejimenti.
Akizungumza kwenye sherehe za uwekaji jiwe hilo la msingi, Mkurugenzi Mkuu wa LabioFarm, Dk. Jose Frag Castro amesema kuwa imekuwa ni heshima kubwa kwa taasisi yake na nchi yake ya Cuba kushiriki katika mradi huu muhimu wa kupambana na ugonjwa wa malaria.
Amesema kuwa katika miaka mitano ijayo, teknolojia 54 mbali mbali kuhusiana na bidhaa ambazo zitazalishwa kwenye Kiwanda hicho zitahamishwa kutoka Cuba kuja Tanzania katika miaka mitano ijayo.