Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa chama hicho kukipigania chama ipasavyo kwa masuala ya kisiasa na kuacha kutegemea Jeshi la Polisi na Serikali kuingilia masuala ya kisiasa. Rais Kikwete ameyasema hayo usiku huu alipokuwa akifunga mkutano Mkuu wa CCM Taifa mjini hapa uliomalizika majira ya saa tano usiku.
Alisema viongozi wa chama wanatakiwa kukisemea chama bila kuchoka hasa kwa masuala ya kisiasa na kuacha kutegemea viongozi wa Serikali na wakati mwingine vyombo vya dola kuingilia masuala ya kisiasa. Alisema yapo maneno mbalimbali ya kipuuzi ambayo yamekuwa yakitolewa na wapinzani dhidi ya CCM, ambayo yanapaswa kujibiwa na viongozi wa CCM wenyewe na si vinginevyo.
Alisema tabia ya baadhi ya viongozi hao kusikia hoja za wapinzani zikitupiwa ndani ya CCM huku wao wamekaa kimya na pengine kuhoji kwanini viongozi wa Serikali hawachukui hatua hazina msingi, hivyo wanapaswa kujibu hoja hizo kisiasa na si kutegemea vyombo vingine.
“Tusitegemee Polisi na Serikali kutusaidia kazi za siasa…mambo ya siasa yanajibiwa na wanasiasa kisiasa, naomba twende tukakisemee chama hili hatulifanyi mara nyingi…tufanye kazi ndani ya chama na nje ya chama,” alisema Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo.
Aidha aliwataka viongozi wa chama kukijenga chama kuanzi ngazi ya chini (kwenye mashina na matawi), ikiwa ni pamoja na kujenga utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na wanachama ili wasaidie kuzifikisha ngazi husika kuwapuzia mzigo wananchi. Aliwataka viongozi na wana CCM kuendelea kutekeleza mradi wa kukiimarisha chama, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuleta mageuzi ndani ya chama ili kukiimarisha chama.
“Tunaondoka leo hapa twendeni tukazibe nyufa za uchaguzi, kuondoa mgawanyiko na mambo mengine ya kipuuzi…,” alisema Mwenyekiti huyo wa CCM aliyechaguliwa tena kwa kishindo na wajumbe. Aliwahakikishia kuwa chini ya uongozi wake atahakikisha CCM inashinda tena kwa kishindo Tanzania Bara na Visiwani uchaguzi mkuu 2015.
Akizungumzia utendaji wa Serikali ya CCM alisema itaendelea kufanya kazi zake kwa uwazi ili kujenga uaminifu kwa wananchi; na kuongeza kuwa hivi karibuni atahakikisha kila waziri anajitokeza kwenye vyombo vya habari na kuzungumza kinachoendelea wizarani kwake pamoja na kujibu maswali ya wananchi baada ya kujieleza.