Rais Kikwete Awang’ang’ania Wezi Vyama vya Ushirika

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitalipa madeni ambayo baadhi ya Vyama vya Ushirika nchini vinadaiwa na mabenki mpaka wezi waliosababisha madeni hayo wamekamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya maofisa wa Serikali hujidhalilisha kwa kujifanya mawakala wa wanunuzi binafsi wa mazao ya wakulima hasa wakati wa msimu wa ununuzi huo. Rais pia amewataka wana-ushirika nchini kuacha kuwachagua wezi kuongoza vyama vyao vingine itafikia hatua ya vyama hivyo kufa kabisa.

Rais Kikwete aliyasema hayo Julai 22, 2014, mjini Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, wakati alipohutubia mkutano wa hadhara na wakati alipozungumza na viongozi wa Mkoa huo ikiwa ni majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani humo. Rais ameondoka Ruvuma, Julai 23, 2014, kwenda Mkoa wa Mtwara.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza katika mkutano wa hadhara wakati anaweka Jiwe la Msingi katika ujenzi wa Barabara yenye sehemu tatu ya Matemanga-Tunduru-Nyakapanya –Mangaka yenye kilomita 195.7 katika sherehe ubwa iliyohudhuriwa na mamia kwa mamia ya wananchi mjini Tunduru.

Rais Kikwete alikuwa anazungumzia maombi ya wananchi wa Tunduru ambao waliomba Serikali ikilipie deni la shilingi bilioni 2.6 ambalo Chama cha Ushirika la TAMCU kinadaiwa na mabenki na hivyo kukifanya kushindwa kununua korosho ya wakulima na kuliachia soko hilo mikononi mwa wanunuzi binafsi ambao wengi wao huwalalia wakulima.

“Nasikitika kuwajulisheni kuwa siko tayari kuidhinisha chama chenu kilipiwe deni mpaka ithibitike deni hilo lilitengenezwa vipi kwa sababu huko nyuma tumepata kulipa madeni yote ya Vyama vya Ushirika kwa kiasi cha kati ya shilingi bilioni 27 na bilioni 30. Nataka kupata maelezo ya uhakika jinsi chama chenu kilivyopata deni hilo – je ni hasara ya kawaida ama ni wizi tu wa viongozi wa chama hicho,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Serikali haiwezi kubebeshwa deni la wezi. Sharti langu kwenu na kwa uongozi wa Mkoa wa Ruvuma ni kwamba kwanza wakamatwe wezi hao na kufikishwa mbele ya sheria na ndipo tuzungumzie kama tunaweza kulipa deni hilo pamoja na kujua ukweli kwamba Serikali ndiyo ilidhamini vyama vya ushirika kukopa. Kazi ya Serikali haiwezi kuwa ni kutumia pesa ya umma kulipa madeni yaliyosababishwa na watu wanaochonga line na kutengeneza madeni. Hatuwezi kufidia wezi.”

Ameongeza: “Kazi kuu ya Vyama vya Ushirika ni kulinda wakulima kwa sababu hivi ni vyama vyao, tena vyama vya hiari. Hivyo, ndiyo walikuwa wanafanya akina Mzee Kahama wa BCU, akina marehemu Bomani wa Victoria na wale wa KNCU. Sasa vyama hivyo vimekuwa sehemu ya kuwadhulumu wakulima.”

“Sasa hata viongozi wa ushirika nao wamekuwa mawakala wa wanunuzi binafsi. Hata maofisa wa Serikali nao wamo. Wanashinda wanazunguka vijijini huko wakati wa msimu kuwafanyia kazi wanunuzi binafsi. Ni jambo la kusikitisha. Hii ndiyo inaeleza kwa nini mfumo wa Stakabadhi Ghalani umekuwa na maadui wengi kwa sababu maadudi hao ni pamoja na maofisa wa Serikali.”