Rais Kikwete Awakemea Viongozi wa Siasa

Rais Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia suala la raslimali za taifa, ikiwamo gesi asilia kujifatufia umaarufu wa kisiasa na kuwapotosha wananchi.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la hatari na lisilo na tija kwa wanasiasa kujaribu kuigawa nchi vipande vipande kwa sababu ya kujitafutia umaarufu kwa kutumia raslimali za taifa.

Rais Kikwete ameyasema hayo Januari 15, 2013 wakati alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini ambaye anamaliza muda wake, Dianne Corner ambaye alifika Ikulu, Dar es Salaam kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi katika Tanzania.

Rais Kikwete na Balozi Corner wamezungumzia masuala mbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza, masuala ya ukanda wa Afrika Mashariki na masuala ya kimataifa.

Kuhusu ugunduzi wa gesi asilia uliofanywa na Kampuni BG ya Uingereza katika eneo la Msimbati kwenye Bahari ya Hindi, walikubaliana kuwa hilo ni jambo jema na lenye kuleta matumaini kwa Tanzania hasa wakati itakapoanza kuvunwa katika miaka michache ijayo.

Kuhusu siasa zilizoanza kujitokeza kufuatia ugunduzi huo mkubwa wa gesi asilia, Rais Kikwete amesema kuwa ni tabia ya hatari kwa wanasiasa kutumia gesi asilia hiyo ama raslimali nyingine kujijengea umaarufu wao ambao umeporomoka.

“Unawezaje kuwa na nchi moja na taifa moja wakati kila mmoja anadai raslimali kutoka kwenye eneo moja ibakie na kunufaisha watu wa eneo hilo tu. Huwezi kuwa na nchi moja na yenye umoja wakati kuna nchi ya gesi asilia kule Mtwara, kuna nchi ya kahawa kule Kilimanjaro, kuna nchi ya chai na ndizi kule Bukoba,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kwa sababu kama gesi asilia inatakiwa kubakia na kunufaisha watu wa Mtwara tu, basi wenye haki zaidi ya kudai jambo hili siyo watu wa Mtwara bali ni watu wa Msimbati ambako ndiko ilipogunduliwa kesi ambako ni maili 60 kutoka Mtwara, kilomita 200 kutoka Newala.”

Ameongeza: “ Unajua nchi yetu inao baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa umaarufu na ambao wanatumia jambo hili jema kwa manufaa yao binafsi bila kujali umoja na jadi ya taifa letu la raslimali zetu kutumika kuiendeleza nchi nzima.”

Kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza, Rais Kikwete amemshukuru Balozi Corner kwa kazi nzuri ya kuimarisha uhusiano huo. “Umeufikisha uhusiano wetu kwenye hatua ya juu kabisa na tunakushukuru kwa jambo hili.”

Corner ambaye amekuwa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania kwa miaka minne amehamishiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).