Na Mwandishi Wetu, Dodoma
RAIS wa Tanzania amesitisha uteuzi wa mawaziri wake wanne, ambao ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha (MB), Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, na Waziri wa Mifugo, Dk. David Mathayo David (Mb).
Rais Kikwete ametengua nafasi za mawaziri hao baada ya kushindwa kusimamia vizuri utendaji kazi wa wizara zao jambo ambalo lilisababisha Oparesheni Tokomeza Ujangili iliyokuwa akizigusa wizara hii kutekelezwa kwa unyanyasaji mkubwa kwa wananchi.
Hata hivyo Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki amewahi kutangaza kujiuzulu mwenyewe bungeni mjini Dodoma ikiwa ni muda mfupi baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuibua hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu mkubwa uliofanya na Oparesheni Maalumu ya Tokomeza ujangili iliyosimamiwa kwa kiasi kikubwa na Wizara yake.
Akizungumza Bungeni kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema Serikali imesikitishwa na vitendo waliotendewa baadhi ya wananchi katika oparesheni hiyo na inatoa pole kwa wote. Alisema Serikali itahakikisha waliohusika na kufanya vitendo hivyo vya kinyama wanawajibishwa ipasavyo ili.
“Vitendo, mauaji ubakaji na unyanyasaji ambao hauwezi kukubalika ipo mifugo imeuwawa vitendo vyote hivyo havikubaliki hata kidogo, dhamira ya oparesheni hii ilikuwa na malengo mazuri lakini tatizo ni namna ilivyotekelezwa.
Hapa ndipo wizara zenyewe zinahusika na kwa kweli mawaziri hawa wote wanne wanapaswa kutanzama na kujipima wenyewe kutokana na kilichotokea…tunaitaji kuwa na tume iliyopendekezwa na Mwanasheria Mkuu iundwe tume ya kimahakama kuchunguza zaidi matukio haya,” alisema.
“Nilizungumza na Waziri mmoja mmoja vizuri baada ya taarifa hizi leo kati ya wote waliohusika, nikijaribu kumueleza kila mmoja hali halisi iliyotokea; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, na Waziri wa Mifugo, Dk. David Mathayo David.
“Nimemtafuta rais nimezungumza naye nimemueleza tukio zima na ameunga mkono hoja hiyo, ya bunge….na akasema mawaziri wote wanne ametengua nafasi zao za uwaziri,” alisema Pinda na kupigiwa makofi na wabunge walio wengi.
Hivi karibuni baada ya wananchi kupitia wabunge wao bungeni kulalamika juu ya vitendo vya mauaji, ubakaji, udhalilishaji, dhuluma na mateso dhidi ya Oparesheni Tokomeza Ujangili iliyokuwa ikiendesha maeneo mbalimbali ya nchi; bunge liliamuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuchunguza tuhuma ukweli wa taarifa hizo na kuishauri Serikali nini cha kufanya.