RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Machi 12, 2015, alifanya ziara maalum ya kutoa pole kwa wahanga wa mvua iliyoandamana na mawe na kusababisha upotevu wa maisha ya watu na uharibifu mkubwa wa mali katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Rais Kikwete amewasili mjini Kahama kiasi cha saa nane mchana baada ya ndege yake kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Mgodi wa Buzwagi na kwa muda wa kiasi cha saa tatu ametembelea familia ambazo zimepata madhara makubwa zaidi kutokana na mvua hiyo iliyonyesha kwa kiasi cha saa moja tu kuanzia saa nne usiku Machi 3, mwaka huu, 2015 na kuambana na upepo mkali na mawe.
Watu 47 walipoteza maisha, 112 wakaumia, nyumba 657 zikabomolewa ama kuharibiwa na kaya 468 kuathirika katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwakata na tokea siku ya maafa, Serikali imetoa huduma za dharura za chakula, sehemu za kulala, huduma za afya na huduma nyingine muhimu kwa binadamu.
Baada ya kupatiwa maelezo ya kina na uongozi wa Mkoa wa Shinyanga chini ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali N. Lufunga, Rais Kikwete ameanzia ziara yake katika Kijiji cha Maghuhumwa, nyumbani kwa Bwana Masemba Maburi, ambaye alipoteza watoto watano katika maafa hayo. Rais Kikwete ametoa pole kwa wafiwa na kuzungumza na wananchi waliokuwepo kwenye msiba.
Bwana Maburi ambaye sasa anaishi katika nyumba ya jirani pamoja na familia yake na familia nyingine tatu amemweleza Rais Kikwete jinsi nyumba mbili ambako watoto hao na mama yao walipokuwa wamelala zilivyoanguka na mama huyo akalazimika kukimbilia nje kwa nia ya kutafuta msaada lakini watoto wakazidiwa na kupoteza maisha.
“Sijawahi kuona mvua kubwa, kali na yenye upepo mkali kiasi kile katika maisha yangu. Mvua ilianza saa nne usiku na ikanyesha kwa muda mfupi sana, nyumba zikaanguka ama kubomolewa. Jameni tusaidie kwa sababu tumekwazika,”Bwana Maburi amemwambia Rais Kikwete.
Baada ya kutoka katika Kijiji cha Maghuhumwa, Rais Kikwete amekwenda katika Kijiji cha Nhumbi ambako amempa pole Bwana Zacharia Limbe na familia yake ambayo ilipoteza wajukuu wanne katika maafa hayo ya mwanzoni mwa mwezi huu.
Akiwa nyumbani kwa Bwana Limbe, Rais Kikwete ametembea na kujionea makazi mapya ya dharura ya familia ambayo yamejengwa kwa msaada wa Serikali.
Baada ya kuondoka kwa Bwana Limbe, Rais Kikwete ametembelea eneo la makazi ya walimu wa Shule ya Msingi ya Mwakata, ambako walimu hao wamehifadhiwa katika fremu za maduka kutokana na athari za maafa hayo. Rais Kikwete amewapa pole walimu hao na kuwaambia: “Pole sana. Tuko pamoja. Tutaendelea kusaidiana kuona jinsi gani mnavyoweza kurejea katika maeneo yenu ya makazi ya kawaida.”