Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameungana na mamia kwa mamia ya waombolezaji katika kuaga mwili wa Kamishna wa Jeshi la Magereza, Elias Mtige Nkuku kwenye shughuli iliyofanyika alasiri ya Januari 13, 2012, katika Viwanja vya Chuo cha Maofisa wa Magereza Ukonga, Dar es Salaam.
Kamishna Nkuku ambaye alikuwa Mkuu wa Fedha na Utawala na hivyo kushikilia nafasi ya pili ya juu katika uongozi wa Jeshi la Magereza nchini alifariki duniani alfajiri ya Januari 11, 2012 kwenye Hospitali ya Regency mjini Dar es Salaam.
Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete amewasili kwenye viwanja vya chuo hicho kiasi cha saa 10 mchana kujiunga na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamshi Vuai Nahodha, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na mamia kwa mamia ya waombolezaji wakiwemo maofisa wakuu, maofisa wadogo na askari wa Jeshi la Magereza kuaga mwili wa Marehemu Nkuku ambaye atazikwa kwao Singida.
Mapema leo asubuhi, Rais Kikwete amefuatana na Mama Salma Kikwete kushiriki katika shughuli za kuuaga mwili wa Kanali Muhangi Pastory Kamugisha zilizofanyika kwenye Viwanja vya Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, Dar es Salaam.
Kanali Kamugisha (P3488) ambaye alifariki dunia Januari 10, mwaka huu wa 2012, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam atazikwa Januari 15, 2012 kwenye Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.