Rais Kikwete Avionya Vyombo vya Habari Kuhusu Uchochezi

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amevitaka vyombo vya habari vya Tanzania kuonyesha ukomavu katika kuisaidia nchi kujenga mahusiano na nchi nyingine badala ya kuandika na kutangaza habari za uhusiano kwa ushabiki na utiaji chumvi.
Wito huo wa Rais Kikwete unafuatia uandishi wa habari za mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed uliofanyika, Novemba 10, 2013, mjini Dar es Salaam.
Baada ya mkutano huo, Amina Mohammed aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Kenya sasa imeelewa vizuri msimamo wa Tanzania kuhusu mchakato wa utengamano ndani ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), hatua ambayo imepongezwa na Rais Kikwete.
Kufuatia hatua hiyo muhimu na sahihi ya Kenya, baadhi ya magazeti yaliyochapishwa leo nchini yametoka na vichwa vya habari kama vile “Kenya yaiangukia Tanzania” na “Kenya yasalimu amri”, vichwa vya habari ambavyo havisemi ukweli, siyo sahihi na ni vya uchochezi na uzandiki.
Ni vichwa vya habari ambavyo haviitendei haki Tanzania wala Kenya. Rais Kikwete hakufurahishwa, na kwahakika, amesikitishwa na vichwa hivyo vya habari.
Tanzania, kupitia hotuba ya Rais Kikwete Bungeni Alhamisi iliyopita ilitoa hoja za kuimarisha Jumuia ya Afrika Mashariki. Kenya imeelewa hoja hiyo ya Tanzania na imefanya uamuzi sahihi na wenye manufaa kwa Jumuia yetu. Hivyo, ni wajibu wa vyombo vya habari nchini kuchangia katika kuimarisha Jumuia badala ya kuandika habari za utengamano kwa namna ya ushabiki usiokuwa na maana na usio na mashiko.