RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Mzee Timothy Apiyo kilichotokea usiku wa Juni 10, 2013, katika Hospitali ya Millpark, Johannesburg, Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.
Rais Kikwete amesema kuwa kifo cha Mzee Apiyo kimeinyang’anya taifa la Tanzania mmoja wa watumishi wa umma hodari na wazalendo waliotumikia umma wa Watanzania kwa uaminifu na uadilifu.
Katika salamu zake kwa Balozi Ombeni Y. Sefue, Katibu Mkuu Kiongozi, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa masikitiko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Mzee Timothy Apiyo ambacho nimejulishwa kilitokea usiku wa jana katika Hospitali ya Millpark, Afrika Kusini.”
“Kwa hakika kifo cha Mzee Apiyo kimelinyang’anya taifa letu mmoja wa watumishi wa umma hodari, wazalendo ambao walitumikia umma wa Tanzania kwa bidii, uaminifu na uadilifu mkubwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika nafasi zote ambazo alizishikilia katika utumishi wa umma ukiwamo Ukatibu Mkuu na Ukatibu Mkuu Kiongozi, Mzee Apiyo alionyesha umakini wa kiwango cha juu ulioongozwa na ushikiliaji wa kuigwa wa misingi ya utumishi wa umma.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Kwa hakika, Mzee Apiyo ataendelea kuenziwa kama mfano wa kuigwa wa utumishi uliotukuka wa umma.”
“Kutokana na kifo hiki, nakutumia wewe Katibu Mkuu Kiongozi salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa familia nzima ya Mzee Apiyo ambao wameondokewa na Baba, Babu na Mhimili wa familia. Napenda kukujulisha kuwa niko nawe na familia nzima ya Mzee Apiyo katika kuomboleza msiba huo. Naelewa machungu yenu katika kipindi hiki kigumu. Nawaombea huruma ya Mwenyezi Mungu muwe na subira ya kuweza kuwavusha kipindi hiki. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweka peponi roho ya Marehemu Timothy Apiyo. Amen.”