RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete, Desemba 9, 2014 ametunuku Nishani ya Ushupavu kwa mfanyabiashara ya kukaanga na kuuza viazi (chips) wa Dare s Salaam, Kassim Saidi Kassim, kwa kitendo chake cha kuokoa wananchi dhidi ya jambazi.
Kassim Saidi Kassim alikuwa mmoja wa watunukiwa 28 wa nishani mbali mbali ambazo Rais Kikwete alitunuku ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za Miaka 53 ya Uhuru. Katika sherehe ya kutunuku nishani iliyofanyika kwenye Bustani za Ikulu, Rais Kikwete alieleza kuwa amemtunuku Bwana Kassim Nishani hiyo kwa sababu ya kitendo cha ushupavu alichokionyesha cha kujitoa mhanga kukabiliana na jambazi mwenye silaha ambaye angeleta madhara makubwa.
Katika maelezo yaliyosomwa kabla ya Rais Kikwete kumtunuku Nishani hiyo, ilielezwa kuwa mnamo Julai 7, mwaka 2013, majira ya saa 3:15 usiku, Kassim akiwa katika eneo lake la biashara, alitokea jambazi akiwa na silaha aina ya bastola na kuanza kuwashambulia wateja kwa kuwapiga makofi na kuwapora mali zao na fedha zao.
Iliendeleza kuelezwa: “Kwa ushupavu mkubwa ulichukua chepe na kumpiga jambazi huyo mara mbili kichwani, kipigo kilichosababisha aanguke na kupoteza fahamu. Kitendo hicho kilifanikisha kukamatwa kwa bastola aina ya Globe ambayo nambari zake zilikuwa zimefutwa ikiwa na risasi tano ndani yake na hivyo kuepusha madhara ambayo yangeweza kusababishwa na matumizi mabaya ya silaha hiyo.”
Kassim anakuwa muuza chips wa kwanza katika historia ya Tanzania kutunukiwa Nishani ya Ushapavu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kassim mwenye umri wa miaka 28 alizaliwa katika Kijiji cha Namwinyu, Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma mwaka 1986. Alisoma na kumaliza elimu yake ya msingi mwaka 2002 katika Shule ya Msingi ya Ilala, iliyoko Wilaya ya Ilala, Dar Es Salaam. Baada ya kumaliza elimu ya msingi, alianza kujishughulisha na biashara ya kukaaga na kuuza viazi (chips) katika eneo la Buguruni Malapa.