Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Klabu ya Soka ya Simba ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini, Mheshimiwa Ismail Aden Rage kuomboleza kifo cha aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa muda mrefu wa klabu hiyo, Mzee Jimmy Daniel Ngonya kilichotokea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tarehe 23 Julai, 2011 kutokana na Shinikizo la Damu.
Katika salamu zake hizo, Rais Kikwete amemuelezea Marehemu Jimmy Ngonya kama kiongozi aliyekuwa na dhamira na aliyefanya jitihada kubwa za kuiendeleza Klabu ya Soka ya Simba ambayo katika uhai wake aliwahi kuitumikia katika nyadhifa mbalimbali ukiwamo Ukatibu Mkuu na Ukatibu Mwenezi wa klabu hiyo.
Aidha, Rais Kikwete amesema Marehemu alikuwa na dhamira ya kuendeleza mchezo wa soka nchini kwa jumla.
“Ninamkumbuka Marehemu Jimmy Ngonya pia kutokana na msimamo wake wa dhati na dhamira yake ya kuendeleza mchezo wa soka ili kuinua kiwango cha mchezo huo hapa nchini, na hatimaye kuliwezesha Taifa letu kuwa miongoni mwa mataifa mengine Barani Afrika yenye viwango vya juu vya soka”, amebainisha Rais Kikwete katika salamu zake hizo.
Rais Kikwete pia ametoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu Jimmy Ngonya kwa kuondokewa na mhimili wa familia, huku akiihakikishia familia hiyo kuwa yupo pamoja nao katika msiba huu mkubwa.
Aidha, Rais Kikwete ametuma salamu za pole kwa wanachama wote wa Klabu ya Soka ya Simba na wapenzi wote wa soka hapa nchini.
Amesema Soka la Tanzania limepata pigo kwa kuondokewa na mtu muhimu ambaye bado alikuwa anahitajika kwa ushauri kuhusu masuala ya soka hapa nchini.