Na Mwandishi Maalumu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mageza S. Mulongo kufuatia vifo vya wanafunzi wanane wa Shule ya Msingi Piyaya wilayani Ngorongoro katika Mkoa wa Arusha.
Rais Kikwete pia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu George Frederick Mbowe aliyefariki nyumbani kwake usiku wa Februari 29, 2012 kutokana na ugonjwa wa Kiharusi.
Akizungumzia vifo vya wanafunzi hao walipoteza maisha Februari 27, 2012 wakati wakijaribu kuvuka Mto Losukutane uliokuwa umefurika kufuatia mvua kubwa zilizonyesha katika sehemu mbalimbali za Wilaya ya Ngorongoro jioni ya siku hiyo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za vifo vya wanafunzi 10 wa Shule ya Msingi Piyaya wilayani Ngorongoro katika Mkoa wako wa Arusha waliosombwa na mafuriko ya Mto Losukutane wakati wakijaribu kuvuka Mto huo”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake. “nimesikitishwa zaidi na taarifa kuwa familia mojawapo katika hizo imepoteza watoto watatu kwa mpigo katika tukio hilo”.
Rais Kikwete amesema tukio hilo limeinyang’anya nchi yetu hazina muhimu ya wasomi wa baadaye ambao hapana shaka Taifa letu lilikuwa linawategemea sana kwa maendeleo yake ya baadaye.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha, Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bwana Mulongo kumfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa familia zote zilizofikwa na msiba huo.
Akiwahakikishia familia hizo kuwa binafsi yuko pamoja nao katika kuomboleza vifo vya wapendwa wao, na amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza vifo vya wapendwa wao.
“Namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema azilaze mahali pema peponi roho za wanafunzi wote waliopoteza maisha yao kutokana na mafuriko ya Mto Losukutane”, amemalizia salamu zake za rambirambi Rais Kikwete.
Akizungumzia msiba wa Marehemu George Frederick Mbowe; Kikwete amesema alimfahamu Marehemu George Mbowe enzi za uhai wake kama mchapakazi hodari aliyelitumikia Taifa lake kwa uzalendo, uaminifu na uadilifu mkubwa katika sehemu zote alizowahi kufanya kazi ikiwa ni pamoja na katika Utumishi wa Umma.
“Enzi za uhai wake, nilimfahamu Marehemu George Frederick Mbowe kama mtu aliyejituma kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yake na mchapakazi hodari”, amebainisha Rais Kikwete katika salamu zake.
Amesema sifa hizo alizionesha alipokuwa katika Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) na hata katika nyadhifa za Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), Mwenyekiti wa PSRC na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Rais Kikwete ametoa pole nyingi kwa familia ya Marehemu George Mbowe kwa kuondokewa na mhimili muhimu wa familia, na amewahakikishia wanafamilia kwamba yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao kwani yote ni mapenzi yake Mola.
Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipumzisha roho ya Marehemu George Frederick Mbowe mahali pema peponi, Amina.