Rais Kikwete Atuma Rambirambi Vifo vya Waandishi Handeni

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu kufuatia vifo vya Waandishi wa Habari wawili na Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Handeni vilivyotokea asubuhi ya tarehe 10 Aprili, 2013 baada ya gari la Halmashauri ya Wilaya ya Handeni walilokuwa wakisafiria kutoka Handeni kwenda Tarafa ya Mzundu, Kata ya Ndolwa Wilayani humo kupata ajali kwa kupasuka matairi na kupinduka katika eneo la Misima umbali wa Kilometa 10 kutoka Handeni Mjini.

Katika ajali hiyo, Mwandishi wa Habari, Hamisi Bwanga aliyekuwa akiliandikia Gazeti la UHURU na pia RADIO ABOOD, na Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Handeni, Mariam Hassan walipoteza maisha papo hapo katika eneo la tukio. Mwandishi wa Habari mwingine, Hussein Semdoe aliyekuwa akiyaandikia Magazeti ya MWANANCHI na NIPASHE alifariki dunia katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni ambako alikuwa amepelekwa kwa matibabu.

Ajali hiyo ilitokea wakati Mkuu wa Wilaya ya Handeni na msafara wake alipokuwa akielekea katika Tarafa ya Mzundu, Kata ya Ndolwa Wilayani Handeni ambako alikuwa Mgeni Rasmi katika Kilele cha Siku ya Upandaji Miti Kiwilaya.

“Nimepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa za vifo vya Waandishi wa Habari, Hamisi Bwanga na Hussein Semdoe, pamoja na Ofisa Uhamiaji wa Wilaya ya Handeni, Mariam Hassan vilivyotokea tarehe 10 Aprili, 2013 wakati wakiwa katika mojawapo ya majukumu muhimu ya maendeleo katika Wilaya yako”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mheshimiwa Muhingo Rweyemamu.

Aidha Rais Kikwete amesema anatambua pengo lililoachwa na Mtumishi wa Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuondokewa na Afisa Uhamiaji wa Wilaya, lakini pia pengo lililoachwa katika Taaluma ya Uandishi wa Habari hapa nchini kutokana na kufariki kwa Waandishi wa Habari wawili kwa mara moja.

“Ninakutumia wewe Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu Salamu zangu za Rambirambi kwa kuondokewa na Mtumishi muhimu katika Ofisi yako. Vilevile Salamu zangu za Rambirambi ziwafikie Waandishi wote wa Habari hapa nchini kwa kupoteza wenzao wawili. Nina hakika mchango wao ulikuwa mkubwa na muhimu katika Taaluma ya Uandishi wa Habari hapa nchini”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

Aidha Rais Kikwete amesema Salamu zake hizo ziwafikie pia Wanafamilia na ndugu wote wa Marehemu, Hamisi Bwanga, Hussein Semdoe na Mariam Hassan kwa kuondokewa ghafla na wapendwa wao. Amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza vifo vya ndugu zao huku akiwahakikishia kuwa yupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza mahala pema peponi Roho za Marehemu wote. Amina

Rais Kikwete amesema anamuomba Mola awape nafuu waliojeruhiwa katika ajali hiyo ili wapone haraka, na awawezeshe kuungana tena na ndugu na jamaa zao, hivyo kuendelea na maisha kama ilivyokuwa kabla ya ajali hiyo.