Rais Kikwete Atuma Rambirambi Msiba wa Jenerali Herman Lupogo

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange kuomboleza kifo cha Meja Jenerali Herman Cornel Lupogo ambaye aliaga dunia Oktoba 19, 2014, akiwa na umri wa miaka 76 katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, ambako alikuwa anapata matibabu.

Katika salamu zake, Kikwete amemweleza Meja Jenerali Lupogo kama mzalendo halisi, ofisa mtiifu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyeitumikia nchi yake kwa moyo wote na wakati wote na ambaye ataendelea kuvikumbusha vizazi vingi vya Watanzania maana halisi ya mapenzi kwa nchi yao.

Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo za rambirambi: “Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa za kifo cha Meja Jenerali Herman Cornel Lupogo ambaye nimejulishwa kuwa alipoteza maisha juzi katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Lugalo. Kwa hakika, taifa letu limempoteza Mtanzania halisi, ofisa mtiifu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ambaye ataendelea kuvikumbusha vizavi vingi vya Watanzania maana halisi ya mapenzi kwa nchi yao.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Tokea alipojiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Julai 23, mwaka 1965 hadi alipostaafu utumishi wake Septemba 11, 1992 baada ya kulitumikia Jeshi kwa miaka 28, miezi minne na siku 13, Meja Jenerali Lupogo alionyesha weledi mkubwa wa kazi ya Jeshi na mapenzi makubwa ya kutumikia nchi yake. Alikuwa Ofisa wa mfano.”

“Nakutumia wewe Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi salamu zangu za rambirambi kuomboleza kifo hiki. Najiunga nawe, maofisa wote wakuu, maofisa wadogo na wapiganaji wote kumlilia Meja Jenerali Lupogo. Napenda mjue kuwa niko nanyi katika msiba huu mkubwa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Aidha, kupitia kwako, napenda kufikisha salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wote wa Meja Jenerali Lupogo kwa kuondokewa na mhimili wa familia yao. Niko nao katika majonzi ya msiba huu mkubwa. Niko nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema roho ya Marehemu Meja Jenerali Herman Cornel Lupogo. Amina.”