RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amezungumza kwa simu na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kumpa pole na kutaka kujua jinsi gani Tanzania inaweza kusaidia kufuatia shambulio la kigaidi kwenye Kituo cha Biashara cha Westgate katika eneo la Westlands, Nairobi, ambako watu 59 wameuawa na wengine 175 wamejeruhiwa.
Rais Kikwete alimpigia simu Rais Kenyatta jioni ya Septemba 21, 2013, kutokea mjini New York, Marekani, mara baada ya kuwasili mjini humo akitokea Toronto, Canada, ambako alifanya ziara ya kikazi ya siku tatu. Katika mazungumzo kati ya viongozi hao, Rais Kikwete amemweleza Rais Kenyatta mshtuko na hasira yake kutokana na taarifa za kusikitisha za shambulio hilo la kigaidi lililofanywa asubuhi ya jana hiyo hiyo.
Rais Kikwete amefuatilia mazungumzo hayo kwa salamu rasmi za rambirambi ambazo Rais Kikwete amemtumia Rais Kenyatta akielezea masikitiko na hasira yake kufuatia mauaji hayo ya watu wasiokuwa na hatia akitaka kujua jinsi Tanzania inaweza kusaidia juhudi za Serikali ya Kenya katika kukabiliana na madhara ya tukio hilo na balaa la ugaidi kwa jumla.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Kikwete amemweleza Rais Kenyatta: “Nimekupigia simu mapema leo kuelezea mshtuko na hasira yangu baada ya kusikia habari za kusitikisha za shambulio la kigaidi lililotokea asubuhi ya Septemba 21, 2013, kwenye Kituo cha Biashara cha Westgate katika eneo la Westlands na kusababisha vifo vya watu 59 na mamia ya majeruhi.”
Katika salamu zake hizo za rambirambi RaisKikwete amesema: “Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa hakika, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kutuma salamu za dhati ya moyo wangu kwako wewe, kwa Serikali ya Jamhuri ya Kenya na kwa familia zote zilizopotelewa na wapendwa wao katika shambulio hili. Sala zetu na pole zetu nyingi ziko pamoja na wale wote ambao wameathiriwa na shambulio hili la kutisha. Aidha, tunawatakia walioumia kasi ya kupona.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Shambulio hili linalenga kuitisha Serikali na Wananchi hodari wa Kenya na kudhoofisha nia yao ya kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kuunga mkono jitihada za kuleta amani katika nchi jirani na yenye matatizo ya Somalia.”
“Kwa maana hiyo, shambulio hilo la woga na lisilo na huruma kabisa dhidi ya watu wasiokuwa na hatia, lazima lilaaniwe na kushutumiwa vikali na wapenda amani wote”.
“Tuna hakika kuwa chini ya uongozi wako imara, Serikali ya Kenya itahakikisha kuwa wote waliohusika kufanya kitendo hiki wanasakwa nakufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kama ambavyo Serikali imepata kufanya huko nyuma,” Rais Kikwete amesisitiza na kuongeza:
“Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanasimama bega kwa bega na kaka na dada zao wa Kenya katika kipindi hiki kigumu. Aidha, Serikali ya Tanzania inapenda kuihakikishia Serikali ya Kenya itaendelea kuiunga mkono na kushirikiana nayo katika kupambana na balaa la ugaidi katika sura zake zote.”