Rais Kikwete Atuma Rambirambi Kifo cha Ali Abdallah Kleist Sykes

Marehemu Mzee Ali Abdallah Kleist Sykes

Na Mwandishi Maalum

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo cha Mzee Ali Abdallah Kleist Sykes, mmoja wa waanzilishi 17 wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na mpigania maarufu wa uhuru wa Tanganyika, ambaye ameaga dunia mchana wa Mei 19, 2013.

Mzee Ali Sykes ambaye alikuwa anashikilia kadi nambari mbili ya Chama cha TANU amefariki dunia majira ya saa saba kwenye Hospitali ya Agakhan mjini Nairobi, Kenya ambako alilazwa wiki mbili zilizopita kwa matatizo ya ugonjwa wa moyo.

Katika salamu zake kwa Balozi Abbas Sykes, mdogo wake marehemu Ali Sykes, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa majonzi makubwa taarifa za kifo cha Mzee wetu Ali Abdallah Kleist Sykes ambaye nimejulishwa kuwa amepoteza maisha yake kiasi cha saa saba mchana wa jana kwenye Hospitali ya Agakhan mjini Nairobi, Kenya.”

Amesema Rais Kikwete: “Mzee Ali Sykes ametoa mchango usiokuwa na kifani na usioweza kupimika katika historia ya kupigania Uhuru wa Tanganyika na hatimaye kupatikana kwa uhuru wa nchi yetu. Haikuwa kazi rahisi kupambana na Wakoloni na bila ya uthubutu wake na wenzake pengine historia ya nchi yetu ingekuwa tofauti na ilivyo sasa.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Hata baada ya kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika, Mzee Ali Abdallah Kleist Sykes aliendelea kutoa mchango wa manufaa kabisa kuhusu jinsi ya kuendesha nchi yetu. Ametutoka wakati tunahitaji sana ushauri, hekima na busara zake.”

“Nakutumia wewe Mzee Abbas Abdallah Kleist Sykes salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako naipa familia nzima pole nyingi kwa pigo hili la kuondokewa na mmoja wa nguzo kuu za familia na Uhuru wa nchi yetu. Ameifanyia nchi yetu mambo mengi na tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi kwa yote aliyotufanyia na kutuachia,” amesema Rais kikwete na kuongeza:

“Napenda mjue kuwa niko nanyi katika msiba huu mkubwa. Najiunga nanyi katika kuombleza kifo cha Mzee wetu na kiongozi wetu. Naelewa majonzi na machungu yenu na namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na subira ya kuhimili kishindo cha msiba huu. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Mzee Ali Abdallah Kleist Sykes. Amin.”