Rais Kikwete atuma rambirambi Dodoma

Siku JK alipomtembelea Mzee Omar Selemani akiwa hospitalini kabla ya kifo chake

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, William Jonathan Kusila kufuatia kifo cha Mzee Omar Selemani ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Mkoa wa Dodoma. Suleiman amefariki dunia hospitalini Februari 9, 2012 alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na kifo cha Mzee Omar Selemani ambaye katika uongozi wake ndani ya Chama chetu alijipambanua kwa ushupavu na busara zake vitu ambavyo vilikuwa bado vinahitajika sana”, amesema Rais Kikwete katika salamu zake.

Rais Kikwete amesema yeye binafsi amewahi kufanya kazi kwa karibu na Mzee Selemani enzi za uhai wake na akabainisha jinsi uongozi wake kwa Chama ulivyosaidia sana katika kukijenga na kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi hususan katika Mkoa wa Dodoma, ameongeza kusema Rais Kikwete.

“Kwa hakika kifo chake kimeleta majonzi na simanzi kubwa si kwa familia yake tu bali pia kwa wana-CCM kote nchini lakini kipekee kwa wana-CCM wa Mkoa wa Dodoma ambao walinufaika moja kwa moja na mchango wake hasa kutokana na uchapakazi wake, uaminifu na uadilifu wake kwa Chama chetu”, ameongeza kusema Rais Kikwete.

“Kutokana na ukweli huo na kwa dhati ya moyo wangu, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Mzee Selemani kwa kuondokewa na mpendwa wao ambaye hapana shaka alikuwa pia nguzo imara na mhimili madhubuti kwa maendeleo na ustawi wa familia”, amesema Rais Kikwete.

Ameihakikishia familia ya Marehemu kuwa yeye binafsi yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na amewaomba wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwa kujua kuwa yote ni mapenzi yake Mola. “Ninamuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Mzee Omari Selemani, Amina”, amemalizia salamu zake za rambirambi Rais Kikwete.