Rais Kikwete atolea maelezo tatizo la ajira.

 

Upungufu wa ajira hususan miongoni mwa vijana ni changamoto kubwa kwa nchi zinazoendelea kwa sababu ya uchumi wake kuwa mdogo na kukua polepole.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameyasema hayo Jumatano wiki hii (15 Juni, 2011) wakati akitoa hotuba yake katika kikao cha 100 cha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, Uswiss.

Tunahitaji kutatua tatizo la ajira ambalo linaongezeka, hasa kwa vijana katika nchi zinazoendelea,ili kulitatua kwa umakini zaidi juhudi za pamoja  zinahitajika baina ya  serikali, jumuiya za wafanyabiashara wa kitaifa na kimataifa, mashirika ya kiraia na washirika wetu wa kimaendeleo” Amesisitiza na kufafanua kuwa  “ Kwa ushirikiano baina ya pande hizi zote kasi ya kuongeza na kutengeneza ajira  itaongezeka katika nchi zinazoendelea”.  Rais Amesema.

Shirika la Kazi Duniani ni shirika ambalo huendesha shughuli zake kwa kanuni ya utatu ambapo hujumuisha viongozi wa kiserikali, viongozi wa vyama vya waajiri na vyama vya wafanyakazi duniani na ujumbe wa kila nchi huhudhuria vikao hivi kwa kuzingatia utatu huu.

Mara baada ya kuhutubia mkutano huu mkuu, Rais pia amepata nafasi ya kuzungumza na viongozi na wawakilishi wa nchi za Afrika wanaohudhuria Mkutano wa Shirika la Kazi na kusisitiza kuwa nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto kuu ya kutengeneza ajira na kwa pamoja bara la afrika linaweza kutengeneza ajira katika ushirikiano wa kikanda na hata kupitia jumuiya mbalimbali za kiuchumi barani Afrika kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Soko la pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA), Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na zingine nyingi barani ambazo kwa pamoja zinaweza kupanua ajira na kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi kwa bara la Afrika.

Rais Kikwete amewaeleza mabalozi, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri barani Afrika juu ya makubaliano ya nchi za jumuiya tatu za EAC, COMESA na SADC kuwa katika kikao chao kilichofanyika mwishoni mwa juma lililopita nchini Afrika ya Kusini, viongozi waliazimia kwa pamoja kuunda muungano mkubwa wa soko huru (Free Trade Area) katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ambapo mambo makubwa matatu yatazingatiwa na kutiliwa mkazo ili  kuharakisha maendeleo na uchumi wa wanachama wa jumuiya hizi.

Maeneo hayo ni kukuza masoko baina ya nchi hizi, miundo mbinu na nishati.

Rais amesema maendeleo haya yanalenga katika kukuza uchumi na hatimaye kuongeza na kutengeneza ajira zaidi.

Rais Kikwete pia ametoa changamoto kwa wananchi wa Afrika kuacha kuwa wanyonge na kudharau maendeleo yaliyokwisha patikana katika nchi zao, amesema inasikitisha unapoona Waafrika wanaongea kwa kujidharau na kujidhalilisha wenyewe bila hata kuona kuwa kufanya hivyo ni kujikosea binafsi.

Tunahitaji kuwa wazalendo na pia kuwa na matumaini na bara letu na juhudi zetu katika kujiletea maendeleo na sio kujidharau wenyewe” Rais amewaasa wawakilishi wa Afrika.

Rais Kikwete amerejea jijini Dar-Es-Salaam jana (16 Juni 2011) jioni.

Mwisho

 

Imetolewa na Premi Kibanga,

Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi.

Geneva-Uswiss.

17 Juni, 2011