Rais Kikwete Atoboa Siri Shutuma za DRC Dhidi ya Tanzania

Rais wa DRC, Joseph Kabila

Rais wa DRC, Joseph Kabila


TANZANIA imesema kuwa ni jambo la kusadikika na kufikirika tu kwa baadhi ya watu kudai kuwa haiko tayari kukabiliana na vikundi vya uasi na ugaidi (negative forces) vilivyobakia vikivuruga amani na kusababisha ukosefu wa utulivu ndani ya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Badala yake, Tanzania inaendelea kuwa tayari kukabiliana na vikundi hivyo, kwa mujibu wa mamlaka ambayo majeshi yake pamoja na yale ya Afrika Kusini na Malawi, yamepewa na Umoja wa Mataifa (UN) ya kuvishambulia, kuvimaliza nguvu na kuvinyang’anya silaha (neutralize and disarm all negative forces) vikundi hivyo vyote.

Nchi hizo tatu zinaunda Brigedi ya Kimataifa ya Force Intervention Brigade (FIB), ambayo ni sehemu ya Majeshi ya UN katika DRC ya United Nations Stabilisation Mission in Congo (MONUSCO), yaliyoko chini ya Luteni Jenerali Alberto Santacruz wa Brazil. Chini ya mamlaka ambayo Brigedi hiyo imepewa na UN, majeshi ya nchi hizo tatu, yana uhalali wa kuvishambulia vikundi vya kiasi katika DRC.

Msimamo huo wa Tanzania umerudiwa tena na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Januari 13, 2015, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Novisise Mapisa-Nqakula, Mjumbe Maalum wa Rais wa Afrika Kusini na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Waziri Nqakula amefuatana na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Mahlobo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akiwatakia mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Tanzania Heri ya Mwaka Mpya wakati wa Halfa ya Mwaka ya Sherry Party iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam, Rais Kikwete aliyaeleza maoni na shutuma dhidi ya Tanzania kuwa ni mambo ya “kudharauliwa”.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Zanzibar, Rais Kikwete amemwambia Bibi Nqakula kuwa msimamo wa Tanzania umekuwa ule ule wa siku zote bila mabadiliko yoyote – yaani kuhakikisha kuwa majeshi na vikundi vyote vya uasi ndani ya DRC vinamalizwa. Rais Kikwete amekuwa Zanzibar tokea jana, Jumatatu, Januari 12, 2015 wakati alipohudhuria sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Wako watu wanaojidai kuwa na uwezo mkubwa wa kusoma na kuelewa zaidi maoni na mtazamo wa Tanzania kuliko hata Tanzania yenyewe ….wanadai kuwa Tanzania haina nia ya kukabiliana na vikundi vya uasi katika DRC. Ni watu wa ajabu kabisa hawa kwa sababu Tanzania, kama zilivyo Afrika Kusini na Malawi, zina askari wake katika DRC chini ya Mamlaka ya Umoja wa Mataifa,” amesema Rais Kikwete.

Ameongeza: “Tumeanza kuifanya kazi iliyotupeleka huko kwa kukisambaratisha Kikundi cha M-23. Tuko tayari kukabiliana na Kikundi cha FDLR (Democratic Forces for the Liberation of Rwanda) na vikundi vingine kama vile ADF na vile vya mgambo kama vile Mai Mai. Kilichotuzuia kuimaliza kazi hii mapema ni kwa sababu FDLR waliomba kujisamilisha wenyewe kwa hiari na wakapewa miezi sita. Sasa muda huo umemalizika.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Hivyo, tuko tayari kwa sababu bado majeshi yetu yako DRC na wala masharti ya UN ya kushiriki katika Brigedia ya Kimataifa hayajabadilika na wala Serikali ya Tanzania haijapeleka maelekezo tofauti kwa majeshi yake mbali na yale yaliyotolewa mwanzoni mwa opereshani hiyo na UN.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Mamlaka ya ushiriki wa majeshi yetu uko wazi, hakuna mchanganyiko wowote katika maelekezo yaliyotolewa kwa askari wote na hakuna maelekezo mapya yaliyotolewa kwa vijana wetu. Wanaendelea na kazi yao.”

Wakati huo huo, Rais Kikwete leo, Jumanne, Januari 13, 2015, ameendesha Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi kwenye ofisi ya CCM, Zanzibar, iliyoko Kisiwandui.