Rais Kikwete Atoa Rambirambi Vifo vya Wananchi na DC Kalambo

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang'a akizungumza enzi za uhai wake.

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Moshi Chang’a akizungumza enzi za uhai wake.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Paschal Mabiti, kuomboleza vifo vya watu 11 ambao wamepoteza maisha katika ajali ya basi iliyotokea mkoani humo, Aprili 21, 2014. Katika salamu hizo, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa ajali zabarabarani zinaendelea kuchukua maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

“Nimepokea kwa huzuni nyingi taarifa ya ajali hiyo ambayo nimejulishwa kuwa imetokea katika Kijiji cha Itwimila katika Wilaya ya Busega katika Mkoa wako wa Simiyu wakati basi lililokuwa linasafiri kutoka Tarime, Mkoa wa Mara kwenda Mwanza kupitia Simiyu lilipoacha njia na kugonga nyumba kabla ya kupinduka.”

Amesema Rais Kikwete: “Nakutumia salamu zangu za rambirambi na najiunga nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa katika nchi yetu. Aidha, kupitia kwako, natuma salamu za dhati ya moyo wangu kwa familia zote ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Naungana nao katika kuomboleza wapendwa wao. Napenda wajue kuwa msiba wao ni msiba wangu. Pia, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aziweke peponi roho za marehemu.”

Rais Kikwete vile vile ametoa pole kwa wote ambao wameumia katika ajali hiyo, akiwaombea wapone haraka na kurejea kwenye shughuli zao za kujiletea maendeleo.

Wakati huo huo Rais Kikwete pia amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda kuomboleza kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa, Ndugu Moshi Chang’a.

“Ni kifo cha kusikitisha kwa sababu kimepunguza safu ya uongozi wetu na kimelinyang’anya taifa letu mhamasishaji hodari na mtetezi wa kuaminika wa maendeleo ya wananchi,” Rais Kikwete amesema katika salamu hizo.
Amesema Rais Kikwete katika salamu zake za rambirambi: “Nilimjua Ndugu Chang’a kwa miaka mingi tokea mwaka 1979 alipojiunga na utumishi wa Chama cha Mapinduzi ambacho pia alikitumia kwa uaminifu mkubwa hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mwaka 2003. Alikuwa kiongozi wa kweli kweli wa maendeleo na kifo chake kimetuachia pengo la uongozi.”

“Nakutumia salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako, naitumia familia wa Ndugu Chang’a pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa na mzazi na mhimili wa familia. Nakuomba uwajulishe kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu kwa sababu yote ni mapenzi ya Mungu. Aidha, naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo.

Ndugu Moshi Chang’a ambaye aliaga dunia jioni ya Aprili 20, 2014 katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Dar Es Salaam amekuwa mkuu wa wilaya katika Mikoa ya Mbeya, Tabora na Rukwa.