Rais Kikwete atoa mada kuhusu muundo wa maendeleo

Rais Jakaya Kikwete, akizungumza.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Juni 20, 2011, alikuwa ni miongoni mwa wakuu wa Serikali na nchi za Afrika waliopewa mada maalum kuhusu Muundo Mpya wa Maendeleo wa Malaysia (New Economic Model for Malaysia) programu zake za utekelezaji.
Mpango huo unalenga kuivusha nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia kutoka kwenye hadhi yake ya sasa ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati na kuwa nchi tajiri ambayo watu wake wana pato ya dola 15, 000 na zaidi kwa mwaka.
Mada hiyo maalum kwa viongozi hao wa Afrika imetolewa na Dato’ Sri Idris Jala, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia, Datuk Sri Mohammed Najib Tun Abdul Razak katika shughuli maalum kwa viongozi hao iliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu huyo katika mji mpya wa Serikali ya Malaysia wa Patrajala, nje ya mji mkuu wa nchi hiyo wa Kuala Lumpur.
Dkt. Jala amewaeleza viongozi hao wa Afrika ambao walikuwa ni pamoja na Rais wa Zimbabwe, Mheshimiwa Robert Gabriel Mugabe na Waziri Mkuu wa Lesotho, Mheshimiwa Pakalitha Bethuel Mosisili katika hatua zote muhimu ambazo nchi hiyo imepitia kuweza kufikia kwenye muundo huo.
Dkt. Jala pia amemwambia viongozi hao kuhusu jinsi wananchi wa Malaysia walivyoshirikishwa katika maandalizi ya muundo huo ambao unalenga kuifanya Malaysia nchi ya dunia ya kwanza katika miaka 10 ijayo, yaani 2020.
Amesema kuwa baada ya muundo na programu zake kuwa vimebuniwa, wadau mbalimbali kiasi cha watu 500 walikusanywa na kuwekwa katika chumba kimoja ili kujadili programu za utekelezaji wa mpango huo na baada ya hapo uliwasilishwa kwa wananchi katika mikutano ya hadhara ili kuwajulisha wananchi kuhusu muundo huo na kutaka maoni yao. Baada ya hapo, muundo huo na programu zake vilichapishwa katika machapisho.
Dkt. Jala amewapitisha viongozi hao katika vipengele muhimu vya muundo huo na progamu zake za utekelezaji ambazo ni pamoja na Programu ya Mageuzi ya Uchumi (ETP) na Programu ya Mageuzi ya Serikali (GTP).
Kaulimbiu kuu ya muundo huo mpya wa maendeleo katika Malaysia ni Big Results Fast, yaani mipango mikubwa ya kuleta matokeo haraka.
Muundo huo na programu zake vitawagharimu wananchi wa Malaysia kwa maana ya Serikali, sekta ya umma na sekta binafsi kiasi cha RM (fedha za Malaysia) bilioni 444 na mipango 131 itakatekelezwa kwa lengo la kubadilisha wananchi wa Malaysia na kuwafanya matajiri.
Dkt. amesema wananchi katika mikutano yao na viongozi walioandaa muundo huo, wananchi walisema kuwa walikuwa na wasiwasi kuhusu kuongeza kwa hali ya uharifu, hali isiyoridhisha ya usafiri wa umma, hali ya elimu, miundombinu ya msingi ya maeneo ya vijijini na hali ya rushwa.
Wakati wa mada hiyo, Rais Kikwete ametaka kujua ni hatua zipi hasa Malaysia ilichukua ili kuondokana na umasikini mkubwa uliokuwa unawakabili wananchi wa nchi hiyo iliyopata uhuru mwaka 1957, sawa na Ghana, kutoka kwa Waingereza.
Dkt. Jala amesema kuwa pamoja na kwamba Malaysia imepiga hatua bado inayo matabaka matatu yaani ya kundi la watu walioendelea, kundi la watu wa kati na kundi la masikini, hasa katika maeneo ya vijijini.
Hata hivyo, alishauri kuwa muhimu ni kwa Tanzania kuamua maeneo gani muhimu ya uchumi yanayoweza kubadilisha haraka maisha ya Watanzania na kuelekeza nguvu kwenye maeneo hayo.
Kwa ushauri, alitaka maeneo la msingi kwa maendeleo ya haraka kuwa ni miundombinu na hasa barabara, elimu na hatua nyingine zinazoweza kuboresha kwa haraka maisha ya watu wa kipato cha chini.
Viongozi hao wa Afrika wako mjini Kuala Lumpur kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa Ushirikiano wa Kimkakati baina ya nchi zinazoendelea wa Langkawi International Dialogue 2011 unaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Putrajaya (PICC). Mkutano huo ulioanza jana unamalizikka kesho, Jumanne, Juni 21, 2011.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
KUALA LUMPUR, MALAYSIA.
20 Juni, 2011