RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa kazi nyingine. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Dodoma, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk. Ibrahim Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Taarifa inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dk. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dk. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara. Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dk. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma, Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dk. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita. Taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kuteua Makatibu Wakuu wanne wapya na kuhamisha mmoja. Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa. Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa walioteuliwa kuwa Makatibu Wakuu ni Dk. Donan Mmbando ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Yohana Budeba ambaye anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mbogo Futakamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Dk. Adelhelm James Meru ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Maliasili.
Kabla ya uteuzi wake, Dk. Mmbando alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Budeba alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Mhandisi Futakamba alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Dkt. Meru alikuwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA). Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amemhamisha Bibi Maimuna Tarishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Kuhusu uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa, Rais Kikwete amemteua Bw. Charles Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Adoh Steven Mapunda, Mkurugenzi Mtendaji, Manispaa ya Bukoba kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Severine Kahitwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dk. Faisal Issa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.
Rais Kikwete pia amemteua Kanali (Mst) Joseph Simbakalia, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA. Uteuzi huo unaanza leo na Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014, Ikulu, Dar es Salaam.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi. Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.