RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Kimataifa ya Kuchunguza Jinsi ya Kugharimia Elimu Duniani – The International Commission on Financing Global Education Opportunity.
Tume hiyo, inayoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown ambaye pia ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN) wa Elimu Duniani ina jumla ya wajumbe 30, wakiwemo marais na mawaziri wakuu wa zamani, wataalum wa elimu, wafanyabiashara kutoka sekta binafsi na wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO’s) duniani.
Tume hiyo imeteuliwa na viongozi watano duniani wakishirikiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na ilitambulishwa kwa mara ya kwanza katika mkutano uliofanyika Septemba 29, mwaka huu, 2015 mjini New York, Marekani.
Rais Kikwete alihudhuria mkutano huo wa kwanza wakati wa ziara hiyo Marekani ambako pia alikuwa anaongoza Jopo ya Watu Mashuhuri Duniani ambao wanaangalia jinsi dunia inavyoweza kujiandaa vizuri zaidi dhidi ya magonjwa ya milipuko.
Viongozi walioteua Tume hiyo ni Mheshimiwa Erna Solberg ambaye ni Waziri Mkuu wa Norway, Michelle Bachelet Rais wa Chile, Irina Bokoba ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Mheshimiwa Peter Mutharika Rais wa Malawi na Mheshimiwa Joko Widodo Rais wa Indonesia.
Tume hiyo ya Elimu itawasiliana na kukutana na viongozi mbali mbali duniani, wabuni sera za elimu na watafiti wa masuala ya elimu ili kuiwezesha Tume hiyo kujenga hoja zinazokidhi umuhimu wa kuwepo kwa upatikanaji wa fedha za kutosha na uwekezaji katika kuleta usawa katika upatikanaji wa nafasi za elimu kwa watoto wa kike na kiume.
Aidha, Tume hiyo italenga kuangalia jinsi gani dunia inavyoweza kuongeza uwekezaji katika elimu katika muda mfupi na katika muda mrefu na itapendekeza aina ya uwekezaji na hatua za kuchukuliwa.
Pia, Tume hiyo itapendekeza njia za kuwashawishi wakuu wa nchi na Serikali, mawaziri wa fedha, uchumi, elimu na ajira, magavana wa majimbo na serikali za mitaa pamoja na viongozi wa kibiashara na wawekezaji kuchukua hatua za kuwezesha ongezeko kubwa la fedha katika sekta ya elimu.
Miongoni mwa watu ambao watatumikia kwenye Tume hiyo pamoja na Rais Kikwete ni Rais wa zamani wa Mexico Mheshimiwa Felipe Calderon, Rais wa zamani wa Kamisheni ya Ulaya Mheshimiwa Jose Manuel Barroso, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dangote Group Bwana Aliko Dangote, Waziri Mkuu wa zamani wa Australia Mheshimiwa Julia Gillard, Rais wa Benki ya Dunia Mheshimiwa Jim Kim, na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Alibaba Group ya China, Bwana Jack Ma.
Wengine ni Mama Graca Machel wa Mozambique, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Econet Wireless Group ya Zimbabwe Bwana Strive Masiyiwa, Mwanamuziki Shakira Mebarak, Waziri wa zamani wa fedha wa Marekani na Rais wa Heshima wa Chuo Kikuu cha Harvard Bwana Lawrence Summers na Bi. Helle Thorning Schmitt, waziri mkuu wa zamani wa Denmark.
Wakati huo huo; Rais Kikwete ameondoka nchini Oktoba 8, 2015 kwenda Mozambique kwa ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili nchini humo kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Filipe Nyusi.
Akiwa nchini Mozambique, Rais Kikwete atatumia nafasi hiyo kuuaga rasmi uongozi wa nchi hiyo na wananchi wa Mozambique wakati anajiandaa kustaafu urais wa Tanzania na kukabidhi madaraka kwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika wiki chache zijazo.
Tanzania na Mozambique ni nchi ambazo zimekuwa marafiki wakubwa na wa damu kwa miaka mingi tokea wakati wapiganaji wa Chama cha Frelimo walipokuwa wakipigania uhuru wa nchi hiyo dhidi ya wakoloni wa Kireno tokea nchini Tanzania ambako chama hicho kilianzishwa mwaka 1964.
Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani kesho baada ya kuwa amemaliza ziara hiyo.