Rais Kikwete Ateuliwa Kujadili Utandawazi Ulimwenguni

Rais Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameteuliwa kuwa miongoni mwa watu wachache mashuhuri duniani ambao watajadili Mawazo na Njia Mpya za Utandawazi wa Usawa na Haki (New Ideas for a Fair Globalisation) na jinsi Utandawazi unavyoweza kuendeshwa kwa usawa zaidi na kunufaisha nchi zote duniani.

Watu hao mashuhuri wameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Ban Ki-Moon na Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Barosso kujadili njia mpya ya Utandawazi wa haki na usawa zaidi katika mkutano (retreat) wa watu wachache utakaofanyika katika Kijiji cha Alpbach, Austria, kuanzia kesho.

Mkutano huo wa siku mbili ambao utakuwa chini ya Wenyeviti Wenza Ban Ki-Moon na Barosso utafanyika chini ya kivuli cha Taasisi ya European Forum Alpbach na Rais Kikwete ni kiongozi pekee wa Afrika aliyealikwa kushiriki katika mkutano huo.

Mbali na kushiriki katika majadiliano ya mada mbali mbali, Rais Kikwete amepangiwa kuzungumza katika kikao cha ufunguzi pamoja na waheshimiwa Ban Ki Moon na Barasso na pia kuzungumza katika kikao cha kufunga mkutano huo na wenyeviti wenzao hao wawili pamoja na Rais wa Muungano wa Austria, Mheshimiwa Dk. Heinz Fischer.

Rais Kikwete aliondoka nchini usiku wa Agosti 28, 2013, kwenda Alpbach tayari kwa mkutano huo ambao mada zake kuu zitakuwa ni Nishati Endelevu na Mabadiliko ya Tabianchi, Usalama wa Chakula na Lishe na Elimu na Vijana.