Rais Kikwete Ateua Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi Tanzania

Kamanda Ernest Mangu akitoa taarifa.

Mkuu Mpya wa Jeshi la Polisi Tanzania, Ernest Mangu akitoa taarifa.


RAIS Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete leo, Desemba 30, 2013, amemteua Kamishna wa Polisi Ernest Mangu kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku wa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa Kamishna Mangu anachukua nafasi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini anayestaafu, Said Mwema.

Kabla ya uteuzi wake unaoanza Januari Mosi, 2014, Kamishna Mangu alikuwa Mkurugenzi wa Inteligensia ya Jinai (Director of Criminal Intelligence) katika Jeshi hilo la Polisi. Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa Rais Kikwete amemteua Kamishna Abdulrahman Kaniki kuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, ambayo ni nafasi mpya katika muundo wa sasa wa Jeshi la Polisi.

Kabla ya uteuzi wake, Kamishna Kaniki alikuwa Kamishna wa Uchunguzi wa Kijinai (Commissioner for Forensic Investigations).
IGP Ernest Mangu ambaye kwa sasa ni Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi ataapishwa Jumanne, Desemba 31, 2013 katika Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.