Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Machi 21, 2012 ameteua Makatibu Tawala wa Mikoa saba na kufanya uhamisho wa wengine watatu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue Makatibu walioteuliwa ni pamoja na Dk. Faisal Hassan Haji Issa, anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Mariam Amri Mtunguja anayekuwa Katibu Tawala wa Mbeya pamoja na Eliya Mtinangi Ntandu anayekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro.
Kabla ya hapo Dk. Faisal alikuwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Rasilimali Watu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, huku Bi. Mtunguja akihudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea na Ntandu akiwa Katibu Tawala Msaidizi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dar es Salaam.
Kwa upande wake Kahitwa kabla ya uteuzi alikuwa Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dodoma, Eng. Kalobelo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmasharui ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, huku Bendeyeko kabla akiwa Kaimu Katibu Tawala Kilimanjaro na Dk. Tarimo akihudumu Ruvuma kama Kaimu Katibu Tawala Mkoa.
Makatibu Tawala wengine na mikoa yao kwenye mabano ni pamoja na Severine Bimbona Marco (Geita), Eng. Emmanuel Kalobela (Katavi), Hassan Mpapi Bendeyeko (Ruvuma) na Dk. Anselem Herbert Tarimo, (Shinyanga).
Aidha Rais Kikwete amesema viongozi hao wataapishwa Ikulu, Jumamosi Machi 24, 2012 saa nne asubuhi na uteuzi wao unaanza rasmi leo Machi 21, 2012.
Walio hamishwa katika taarifa hiyo ni Mgeni Baruani aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro na kuhamishiwa Mkoa wa Njombe, Mwamvua Jilumbi aliyekuwa Katibu Tawala Shinyanga na sasa anahamishiwa Mkoa wa Simiyu pamoja na Bertha Swai, anayehamishiwa Mkoa wa Pwani akitokea Mbeya.