Rais Kikwete Ateta na Watanzania Waishio Zambia

RAIS KIKWETE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa jana, Jumatano, Februari 25, 2015, amekutana na kuzungumza na mamia ya Watanzania waishio nchini Zambia, ikiwa sehemu ya ziara yake rasmi ya siku mbili ya Kiserikali katika nchi hiyo.
Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete alikutana na Watanzania hao usiku kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia, ambako alipata nafasi ya kujibu maswali yao na kuelezea kwa undani mafanikio ya maendeleo ambayo yanaendelea kupatikana nchini.
Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza wa nje kualikwa kutembelea rasmi Zambia tokea Rais mpya wa nchi hiyo, Mheshimiwa Edgar Chagwa Lungu kushika madaraka ya dola mwezi uliopita, hatua inayoonyesha hali ya uhusiano mzuri katika ya nchi hizo mbili jirani na marafiki.
“Ukisoma magazeti yetu nchini na kufuatilia mijadala kwenye mitandao ya kijamii utadhani kuwa hakuna kinachofanyika na kuwa nchi nzima inaongelea katika siasa tu. Lakini tunaendelea kufanya mambo mengi iwe katika elimu, katika afya, kukabiliana na malaria na magonjwa wengine makubwa, kupambana na ukimwi, kusambaza umeme vijijini, mapambano dhidi ya ujambazi na majambazi, shughuli za miundombinu na ujenzi wa barabara pote tunafanya vizuri sana,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Wakati Serikali yangu inaingia madaraka ni asilimia 10 tu ya vijiji vyetu vilikuwa na umeme, sasa tunazungumzia asilimia 45 ya vijiji vya Tanzania vina umeme. Hapa tunazungumzia kiasi cha vijiji 5,000 kati ya vijiji 12,000 vya nchi yetu. Kwa ujumla, asilimia ya usambazaji umeme katika nchi yetu imepanda kutoka asilimia 10 ya mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 36 kwa sasa. Siyo mafanikio madogo hata kidogo.”
Kuhusu hali ya ujambazi nchini, Rais Kikwete amesema kuwa upo ujambazi katika Tanzania, kama ilivyo kwa nchi zote duniani. “Lakini, hawa tutapambana nao hawawezi kutushinda nguvu, tutazama nao na tutaibuka nao tu.”
Rais Kikwete pia ameelezea upanuzi mkubwa wa sekta ya elimu ikiwa ni elimu ya awali, ya sekondari na ya juu. “Katika elimu ya juu, kwa mfano, wakati tunaingia madarakani idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vyote ilikuwa ni 40,000 tu lakini sasa tunazungumzia wanafunzi 200,000.”
Katika afya, Rais Kikwete ameelezea uboreshaji mkubwa wa hospitali za mikoa na ujenzi wa huduma nyingine za afya zikiwemo zahanati na vituo vya afya katika vijiji na kata nchini.
Aidha, Rais Kikwete amezungumzia hatua za kuongeza idadi ya madaktari nchini akisema kuwa kwa sasa idadi ya madaktari wapya kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili wameongezeka kutoka 200 hadi 400 kwa mwaka na kuwa idadi hiyo itakuwa kubwa zaidi wakati ujenzi wa Hospitali ya Mlongazila, nje tu ya Dar es Salaam, utakapokamilika.
Rais Kikwete pia alijibu maswali manane ya Watanzania hao ikiwa ni pamoja na lile kuhusu uraia pacha, misamaha ya kodi kwa Watanzania wanaorejea nyumbani, mikopo kwa wanafunzi wa kike wa Kitanzania ambao wanasomea masomo ya sayansi nje ya nchi, uwezekano wa Benki ya CRDB kufungua tawi katika Zambia, hatua za Serikali kupunguza idadi ya vizuizi vya barabarani, uwezekano wa Watanzania waishio nje kupata nafasi ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na jinsi gani Serikali ya Tanzania inaweza kuwasaidia Watanzania waishio Zambia kufanya shughuli zao kwa uhuru zaidi.