Rais Kikwete ateta na Dk. Mahathir
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye Hoteli iitwayo Prince Hotel and Residence mjini Kuala Lumpur ambako Rais Kikwete amefikia katika ziara yake ya siku nne nchini Malaysia, viongozi hao wawili wamezungumzia masuala yanayohusu uchumi na yale yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Malaysia.
“Tanzania inaendeleaji?”ndilo lilikuwa swali la kwanza la Dk. Mahathir kwa Mheshimiwa Kikwete mwanzoni mwa mkutano huo wa kiasi cha dakika 40.
Rais Kikwete ametumia muda mwingi wa mkutano huo kumweleza Mheshimiwa Mahathir kuhusu Mpango wa Maendeleo mpya ambao Tanzania imeupitisha karibuni na mkakati wa utekelezaji wake.
Kuhusu uchumi, Rais Kikwete amemweleza Mheshimiwa Mahathir kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania akimfahamisha kuwa mfumuko wa bei umeshuka na kuwa chini ya asilimia 10, uchumi wa Tanzania sasa unakua kwa wastani wa asilimia saba, pato la Mtanzania sasa ni wastani wa dola za Marekani 525 na nchi sasa ina fedha za kigeni za kuagiza bidhaa na huduma kwa kiasi cha miezi sita.
Rais Kikwete pia amemwelezea Mzee Mahathir kuhusu hali ya elimu na uwekezaji na kumwomba atumie uzoefu wake kuyashawishi makampuni ya Malaysia kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Viongozi hao wawili wamejadili na kukubaliana kuwa ukosefu wa ajira na kazi ni tatizo kubwa katika nchi zote mbili, Tanzania na Malaysia, na wamekubalina umuhimu wa kuchukua hatua kubwa na za haraka kupambana na tatizo hilo.
Rais Kikwete amemweleza Mheshimiwa Mahathir kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kulitafutia majawabu tatizo hilo, akisisitiza kuwa pamoja na kukua kasi kwa baadhi ya sekta za uchumi bado sekta zinazokua kwa kasi zaidi hazihusiki moja kwa moja na jitihada za Serikali za kupambana na ukosefu wa ajira na umasikini.
Rais Kikwete yuko mjini Kuala Lumpur, Malaysia kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa taasisi ya maendeleo ya Langkawi International Dialogue 2011 uliofanyika kwenye mji mpya wa makao makuu ya Serikali ya Malaysia wa Putrajaya. Mkutano huo ulioanza Jumapili umemalizika leo, Jumanne, Juni 21, 2011.
Imetolewa na:
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
KUALA LUMPUR, MALAYSIA.
22 Juni, 2011