Na Joachim Mushi
RAIS Jakaya Kiwete jana ametembelea ziara katika eneo la Magwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kukagua miundombinu katika eneo hilo ambalo litakuwa makazi ya watu walioathiriwa na mafuriko katika maeneo ya mabondeni.
Akiwa eneo la tukio Rais Kikwete alisomewa taarifa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki juu ya mchakato unavyoendelea na hivyo kutoa maagizo kwa wasimamizi wa zoezi la kuwahamisha waathirika hao kutoweka miundombinu mibovu kwani hali hiyo inaweza kuleta madhara tena kwa wakazi hao hapo baadaye.
Mkuu huyo wa mkoa amemweleza Rais Kikwete kuwa tayari kuna familia 653 ambazo zinatarajia kuhamishiwa katika eneo hilo na kwamba jumla ya viwanja 629 vimeshakamilika. Hata hivyo, Rais Kikwete ametoa agizo kwa Kampuni ya Maji Safi na Majitaka (DAWASCO) kuhakikisha inaweka miundombinu ya maji kulingana na idadi ya watu.
Wakati huo huo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ameitaka Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuharakisha ujenzi wa madaraja na barabara zilizoharibika kutokana na mafuriko yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40 na uharibifu wa miundombinu.
Mnyika ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya siku moja aliyoifanya katika kata za Mbezi, Msigani, Saranga na Kimara zilizoko jimboni humo kuangalia kama Serikali imetimiza ahadi ya kutoa fedha za mpango wa dharura wa kutengeneza barabara na madaraja hayo.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, ilizitaka manispaa zote za jiji kuandika taarifa ya namna zilivyoathirika na kuweka tathmini yake, ambapo manispaa ya Kinondoni ilitoa tathmini ya zaidi ya sh. bilioni moja kuwa zinahitajika kutengeneza madaraja na barabara zilizoharibika.
Hata hivyo Mnyika amesikitishwa na Serikali kushindwa kutimiza ahadi ya kutoa fedha za mpango wa dharura wa kutengeneza miundombinu hiyo ambayo mpaka sasa haipitiki kutokana na uharibifu mkubwa uliotokea.