Rais Kikwete ataka ushirikiano na Uingereza kimaendeleo

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameielezea Uingereza kama mshirika kakati (strategic partner) katika maendeleo ya Tanzania kutokana na miaka 50 ya ushirikiano na misaada ya maendeleo na ya kiufundi kutoka kwa nchi hiyo.

Aidha, Rais Kikwete ametaka nchi zote mbili, Tanzania na Uingereza, kuongeza jitihada za kuvutia uwekezaji zaidi katika Tanzania kutoka Uingereza ambao thamani yake kwa sasa inafikia dola za Marekani bilioni 1.8 (sawa na sh. bilioni 3060).

Rais Kikwete ameyasema hayo usiku wa jana, Jumatatu, Novemba 8, 2011, Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa Chakula cha Kitaifa alichomwandalia Mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles ambaye anatembelea Tanzania na mkewe, Mama Camilla. Prince Charles na Mama Camilla wako kwenye ziara ya siku tatu nchini Tanzania.

Rais Kikwete amesema kuwa ziara ya Prince Charles imetoa nafasi kwa Tanzania kuwashukuru wananchi wa Uingereza kwa misaada yao mikubwa ambayo kwa miongo mitano iliyopita wametoa kuchangia maendeleo ya Tanzania.

“Misaada ya Serikali ya Malkia na wananchi wa Uingereza imekuwa muhimu sana katika jitihada zetu za kujikomboa kutoka umasikini na kuelekea katika maisha bora zaidi. Katika miaka 50 iliyopita mumekuwa nasi katika nyakati za raha na nyakati za shida na wananchi wa Tanzania wamenufaika sana kutoka na misaada ya maendeleo na ya ufundi kutoka Uingereza,” Rais Kikwete amemwambia Prince Charles na ujumbe wake.

Ameongeza Rais Kikwete katika hotuba yake fupi: “Misaada muliyotupa imesaidia sana kuboresha kiwango cha maisha ya Watanzania wengi. Imeleta tofauti kubwa katika maisha ya wananchi wetu.”

Rais kikwete amesema kuwa mbali na Uingereza kuwa chanzo kikubwa zaidi cha misaada ya maendeleo na ya kiufundi, nchi hiyo pia imekuwa chimbuko kubwa zaidi la mitaji inayoingia katika uchumi wa Tanzania.

“Ninayo furaha kusema kuwa mbali na kuwa chanzo kikubwa zaidi cha misaada ya maendeleo na ufundi, Uingereza pia imekuwa nchi inayoongozwa kwa kuleta uwekezaji na mitaji katika nchi yetu. Kwa sasa uwekezaji kutoka Uingereza unafikia dola za Marekani bilioni 1.8. Lakini utakubaliana nami kuwa kwamba tunaweza kufanya vizuri zaidi kuliko tulipo na lazima tulenge kufanya vizuri zaidi. Kwa hakika, Uingereza ni mshirika kakati wa maendeleo yetu,” Rais Kikwete amesema.

Prince Charles yuko nchini kwa mwaliko wa Serikali kwa ajili ya kushiriki katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Alikuwa Prince Philip (Duke of Edinburgh), baba yake Prince Charles, ambaye alimkabidhi funguo za Uhuru wa Tanzania Bara Mwalimu Julius Nyerere, waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru na Baba wa Taifa la Tanzania.