RAIS atoa changamoto sekta binafsi kujihusisha zaidi na mapambano dhidi ya Ukimwi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka sekta binafsi kujihusisha zaidi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa sababu ugonjwa huo unaathiri uchumi na biashara na kuongeza mzigo wa gharama za uzalishaji wa makampuni hayo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa pamoja na kwamba Tanzania imekuwa inapata michango mikubwa kupambana na UKIMWI kutoka kwa washirika wake wa maendeleo, bado jukumu la msingi la kupambana na ugonjwa huo nchini ni la Watanzania wenyewe.
Pia, Rais Kikwete amewakumbusha Watanzania kuwa UKIMWI hauna tiba ya kisayansi ama tiba mbadala ya waganga wa jadi ama wapiga ramli kama baadhi ya Watanzania wanavyopenda kujiaminisha. Rais Kikwete alikuwa anazungumza hayo usiku wa kuamkia, Jumamosi, Mei 3, 2014, wakati alipokuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya uzinduzi wa uchagishaji fedha za kupanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya mapambano ya UKIMWI kwa mwaka huu wa 2014 kwenye Hoteli ya Hyatt Regency mjini Dar es Salaam.
Rais Kikwete amewaambia washiriki wa hafla hiyo: “Tumefanikiwa sana kuhamasisha Serikali na wananchi kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI. Hata hivyo, hamasa hii haijaingia sawa sawa miongoni mwa ndugu zetu wa sekta binafsi, ambao ndio waajiri wakubwa kuliko hata Serikali. Upo ushahdi wa kutosha kuwa wao wanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na UKIMWI kwa sababu ugonjwa huo huathiri uchumi na biashara kwa kuongeza mzigo wa gharama za uzalishaji wa makampuni.”
Ameongeza Rais Kikwete: “ Uzoefu kwingineko Barani Afrika na haswa Afrika Kusini, unaonyesha kuwa uwekezaji wa sekta binafsi katika mapambano dhidi ya UKIMWI ni muhimi sana kwao na kwa uchumi wa nchi. Ni gharama ndogo zaidi kwao kupambana na UKIMWI kuliko gharama za kuupuzia, ambazo huishia kuwa kubwa zaidi kwa mwajiri.”
Rais amesema kuwa wajibu wa msingi wa kupambana na UKIMWI nchini ni wa Watanzania na hivyo Watanzania hawana budi kuendeleza mapambano hayo hata pasipo na ufadhili.
“Wajibu wa msingi wa kusimamia mapambano dhidi ya UKIMWI na kuwahudumia wale walioathirika ni jukumu letu sisi Watanzania wenyewe. Hivyo, hatuna budi kuendeleza mapambano hata pale pasipo na ufadhili. Njia pekee ni kuongeza jitihada za ndani kwa kuunganisha nguvu zetu kwenye utafutaji wa raslimali fedha.”
Uchangishaji huo chini ya Kili Challenge 2014 huendeshwa kwa pamoja na Kampuni ya Anglo Gold Ashanti kupitia kampuni tanzu yake ya uchimbaji dhahabu ya Geita Gold Mine (GGM) ya Mkoa wa Geita na mwaka huu ni mara ya 12 tokea kuanzishwa uchangishaji wa fedha za kuunga mkono mapambano ya UKIMWI.
Kiasi cha shilingi bilioni 12 zimechangwa katika miaka hiyo 12 na kiasi cha makampuni 30 yasiyokuwa ya kiserikali na yanayojihushisha na mapambano dhidi ya UKIMWI yamenufaika. Aidha, katika miaka hiyo 12 kiasi cha watu 500 wameshiriki kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha mapambani dhidi ya UKIMWI.
Mwaka huu, kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zinatarajiwa kukusanywa na hadi jana kiasi cha wachangiaji 50 walikwishajiandikisha. Katika shughuli ya usiku huo, Rais Kikwete alitoa hundi za kiasi cha shilingi milioni 700 kwa taasisi mbali mbali kutokana na fedha zilizokusanywa mwaka jana chini ya mpango huo wa Kili Challenge.