Rais Kikwete Ashiriki Mazishi ya Askofu Aloysius Balina

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akiweka udongo kwenye kaburi la Askofu Aloysius Balina wakati wa mazishi ya Askofu huyo kwenye Kanisa la Mama wa Huruma, mjini Shinyanga.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho akitia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki la Shinyanga baada ya kuwasili kwenye Kanisa la Mama wa Huruma katika Parokia ya Ngokolo mjini Shinyanga kushiriki mazishi ya Askofu huyo Jumamosi ya Novemba 10, 2012. Picha zote na Ikulu.

Na Mwandishi Maalumu, Shinyanga

RAIS wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameungana na mamia kwa mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki kumzika Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Baba Askofu Aloysius Balina yaliyofanyika kwenye Kanisa la Mama wa Huruma, Parokia ya Ngokolo, mjini Shinyanga.

Rais Kikwete ambaye aliwasili Shinyanga akitokea Dodoma ambako anaendesha vikao muhimu vya Chama Cha Mapinduzi amewasili kwenye Kanisa hilo saa sita mchana kwa ajili ya mazishi ya Askofu Balina ambaye alifariki dunia Novemba 6 mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa, Mwanza kwa ugonjwa wa saratani.

Mara baada ya kuwasili Kanisani hapo, Rais Kikwete ametia saini kitabu cha maombolezo na kujiunga na viongozi wa Kanisa hilo na wa Serikali akiwamo Rais Mstaafu Mheshimiwa Banjamin Mkapa na Mama Maria Nyerere kushiriki katika mazishi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.

Kabla ya kutoa salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amesikiliza salamu za rambirambi za Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedict wa 16, na pia amesikiliza Amri ya Kitume ya Kuhani Mkuu huyo wa Kanisa hilo, iliyotangaza kuteuliwa kwa Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Mhashamu Juda Thaddeus Ruwa’ichi kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Shinyanga hadi atakapoteuliwa askofu mpya wa jimbo hilo.

Amri hiyo imetolewa na kutiwa saini na Katibu wa Kongresio ya Uinjilishaji wa Kimataifa na Rais wa Jumuiya ya Kazi za Kipapa Duniani, Askofu Mkuu Protase Rugambwa na kusomwa na Balozi wa Baba Mtakatifu katika Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla.

Katika salamu zake zake za rambirambi ambazo amezielekeza kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tracisius Ngalalekumtwa na waumini wa Kanisa Katoliki, Rais Kikwete amemwelezea Askofu Balina kama kiongozi mwadilifu na mchapakazi ambaye hukuchoka katika maisha yake kutumia nafasi zake mbali mbali alizozishikilia katika maisha yake kuwasaidia binadamu wenzake. Rais Kikwete pia ameelezea jitihada ambazo yeye na Askofu Balina walizifanya katika kusaka fedha za kupanuliwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko Mwanza.

Baada ya kutia udongo kwenye kaburi la Askofu Balina na kuweka shada la maua kwenye kaburi hilo, Rais Kikwete alimpa pole na kumfariji Bibi Theresia Nago ambaye ni mama yake mzazi Askofu Balina kabla ya kuondoka Kanisani hapo.

Askofu Balina alikuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga nafasi aliyoishikilia kwa miaka 16 na kabla ya hapo alikuwa Askofu wa Jimbo la Geita kwa miaka 12. Askofu Balina alikuwa askofu kwa miaka 28 na padre kwa miaka 41.

Aidha, Askofu Balina alikuwa Mkuu wa Idara ya Afya ya TEC kwa miaka mingi na pia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali ya Bugando. Rais Kikwete alirejea mjini Dodoma jioni ya Novemba 10, 2012 kuendelea na vikao vyake vya CCM.