Rais Kikwete asema Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu 2015 chini ya Katiba Mpya

Rais Jakaya Kikwete (wa kwanza kushoto) akizungumza na wazee jijini Dar es Salaam jana kwa kulihutubia Taifa zima kupitia radio na televisheni mbalimbali. (Picha na Full Shangwe Blog)

Na Joachim Mushi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema atahakikisha nchi inafanya unyaguzi mkuu ujao ikiwa na katiba mpya inayokidhi hali ya mabadiliko ya sasa. Amewataka wananchi na wadau wengine katika makundi yao wajiandae kutoa maoni yao katika mchakato wa uundaji katiba mpya pale utakapo kamilika.

“Lengo letu ni kuwa ifikapo mwaka 2014 zoezi zima liwe limekamilika ili mwaka 2015 tufanye uchaguzi tukiwa na Katiba mpya. Itapendeza tukisherehekea miaka 50 ya Muungano na Katiba mpya. Ni matumaini yangu kwamba wananchi wote watashiriki kwa ukamilifu kutoa maoni yao kwa Tume hiyo,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni utaratibu wake wa kulihutubia Taifa. Katika hotuba hiyo ambayo kiasi kikubwa amefafanua mchakato wa uundaji katiba mpya na muswada uliowasilishwa bungeni juu ya kuhalalisha mchakato mzima, Rais Kikwete amesema anashangazwa na baadhi ya watu kutoitambua nia njema ya Serikali kwa kuamua kuanza mchakato wa uundaji Katiba Mpya.

Amesema mchakato unaoendelea sasa juu ya uundaji wa sheria itakayosimamia muundo wa Katiba Mpya umefuata taratibu zote kisheria chini ya Katiba iliyopo hivyo ni lazima uheshimike tofauti na upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya vyama vya upinzani na wanaharakati.

Amesema kwa mujibu wa Katiba iliyopo Rais hawezi kujiondoa katika mchakato wa uundaji wa Katiba mpya kwa kuwa amepewa mamlaka hayo kisheria.

“Kama mtakavyokumbuka tarehe 31 Desemba 2010 katika hotuba yangu ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 nilizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2011. Miongoni mwa mambo ambayo niliyataja kuwa tutayafanya katika kusherehekea siku hiyo adhimu ilikuwa ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa nia ya kuihuisha ili hatimaye tuwe na Katiba mpya.”

“Nilifafanua siku ile kwamba tunataka kufanya hivyo si kwa sababu Katiba yetu ya sasa ni mbaya, la hasha! Nilieleza kwamba Katiba yetu ya sasa ni nzuri na imelilea vyema taifa letu. Tuna nchi yenye amani, utulivu na umoja pamoja na watu wake kuwa wa rangi, makabila, dini na itikadi mbalimbali za kisiasa.”

“Tunayo nchi ambayo imepiga hatua kubwa sana ya maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa miaka 50 iliyopita. Pamoja na hayo tunataka kuihuisha Katiba yetu ili tuwe na Katiba inayoendana na Tanzania ya miaka 50 baada ya Uhuru wa Tanzania Bara, Tanzania ya miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Tanzania ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema Kikwete katika hatuba yake.

Aidha alisema dhamira ya yeye kuunda Tume Maalum ya Katiba yaani ‘Constitutional Review Commission’ itakayojumuisha Watanzania wa makundi mbalimbali katika jamii yetu na kutoka pande zetu mbili za Muungano ni kutoa mwongozo na kuratibu mchakato wa kupata maoni ya Watanzania kuhusu nini wanakitaka kwenye katiba mpya.

Amesema tume hiyo itakuwa na kazi ya kusikiliza maoni ya wananchi na baadaye kutengeneza rasimu ya Katiba mpya ambayo baada ya kukubaliwa na Bunge itafikishwa kwa wananchi kutoa ridhaa yao kwa kupiga kura.

Hata hivyo alisema si mara ya kwanza kwa rais kufanya zoezi la marekebisho ya Katiba au hata kuandika upya Katiba tangu Uhuru na Muungano, kwani hata huko nyuma mara zote Tume ya kukusanya maoni ya wananchi iliundwa na Rais.

“Ndivyo ilivyokuwa wakati wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa tatu Mzee Benjamin Mkapa. Mwalimu Julius Nyerere alifanya hivyo mara tatu. Mara ya kwanza mwaka 1963 wakati wa kubadilisha mfumo wa vyama vingi kwenda Chama kimoja, Rais aliunda Tume ya Mheshimiwa Rashid Kawawa, Amon Nsekela. Mara ya pili wakati wa kutengeneza Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 aliunda Tume ya Mzee Sheikh Thabit Kombo,” alifafanua Rais Kikwete.

Ameongeza kuwa jambo lingine lililopotoshwa ni dhana ya muswada kusomwa mara ya kwanza bungeni. Akifafanua zaidi alisema kwa mujibu wa utaratibu wa kutunga sheria, Miswada, husomwa mara tatu Bungeni- na muswada kusomwa mara ya kwanza ni pale unapogawiwa kwa Wabunge baada ya kuchapishwa katika gazeti la Serikali siku 21 kabla ya kuwasilishwa Bungeni.

“Muswada huu ulisomwa mara ya kwanza mwezi Aprili na kupelekwa kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala mwezi Aprili, 2011. Tangu wakati huo Kamati imekuwa ikiufanyia uchunguzi Muswada huo na kukusanya maoni ya wadau. Walisikiliza wadau Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na kufuatilia maoni ya makongamano, magazetini na kwenye mitandao. Kisha Kamati ikayajadili na kutoa mapendekezo yake ambayo Serikali iliyasikiliza na kuyajumuisha wakati uliposomwa mara ya pili. Muswada huu haukuwahi kuondolewa Bungeni. Kwa sababu hiyo, hakuna sababu ya kurudia kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa taratibu za kuendesha Bunge,” alisema Rais Kikwete.

Akielezea hali ya uchumi wa nchi Rais Kikwete alisema mfumuko wa bei, uliopo sasa umechangiwa kwa asilimia kubwa na hali ya uchumi wa mataifa ya Marekani, Ulaya Magharibi na Japan- hali ambayo imesababishwa na machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa miaka miwili iliyopita.

“Ni vizuri tukafahamu kuwa, matatizo ya mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha yetu siyo yetu peke yetu. Nchi zote za Afrika Mashariki zinakabiliana na matatizo haya. Kwa mfano, mfumuko wa bei kwetu ni asilimia 17.9, Kenya wako asilimia 18.9 na Uganda asilimia 30.5. Wakati mwaka wa jana sote tulikuwa kwa watani karibu asilimia 5. Kwa upande wa kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola sote tumeathirika. Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 9.4, Kenya kwa asilimia 6.8 na Uganda kwa asilimia 17.4. Randi ya Afrika Kusini kwa asilimia 18.7, Rupia ya India kwa asilimia 9.8, Pauni ya Uingereza kwa asilimia 6.6. na Euro kwa asilimia 9.7,” alisema Rais.